FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe, Adam Kighoma Malima, amewataka watumishi wa umma pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutengeneza mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji, ili kuvutia uwekezaji utakaosaidia kukuza sekta mbalimbali za uchumi Mkoani Morogoro.
Akizungumza katika mkutano wa wawekezaji Malima amesema kwamba uwepo wa wawekezaji katika sekta mbalimbali ni chanzo cha maendeleo ya haraka kwa Mkoa wa Morogoro na taifa kwa ujumla.
Aidha amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa ushirikiano ili kurahisisha uwekezaji na kutatua changamoto zinazozuia maendeleo ya sekta binafsi.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge, amesema kuwa Kwa Mkoa wa Morogoro hadi sasa miradi 314 imesajiliwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda, usafirishaji na nyinginezo.
Mahenge alieleza kuwa hii imesaidia kupanua wigo wa ajira na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi.
Mkutano huo ulilenga kuhamasisha uwekezaji endelevu, huku pia ukitoa wito kwa wawekezaji wakubwa kutambua fursa zilizopo na kuwekeza kwa wingi, ili kuendeleza uchumi wa Mkoa wa Morogoro na kuongeza ajira kwa wananchi.