Mlezi wa kituo cha Watoto Wetu Tanzania,Gerald Soka akiwashukuru Wazee wastaafu wa TRA waliofika kwenye kituo hicho kutoa msaada wao.
Lucas Kaigarula mwanachama wa kundi la Wastaafu wa TRA pia Mratibu wa ziara ya utoaji msaada katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Watoto wetu Tanzania kilichopo Mbezi eneo la Goba jijini Dar es Salaam. Akizungumza na waandishi wa habari muda mchache baada ya kukabidhi mahitaji kwa watoto hao
Erina Misso Mweka hazina wa Kundi la Wastaafu wa TRA akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa msaada wao kwenye kituo cha watoto yatima cha Watoto Wetu Tanzania kilichopo Mbezi ebeo la Goba, Dar es Salaam
Yeremiah Mbaga Katibu wa Kikundi cha Wastaafu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa mchango wao kwenye kituo cha kulea watoto yatima cha Watoto wetu Tanzania kilichopo Mbezi eneo la Goba, Dar es Salaam
WAZAZI na walezi wameaswa kushikamana kuwalea watoto katika malezi bora ili kuwaepusha watoto kukimbilia kulelewa kwenye vituo vya watoto yatima.
Hayo yameelezwa Februari 22, 2025, wakati kikundi cha Wastaafu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), walipotembelea kituo cha kulelea watoto cha Watoto Wetu Tanzania kilichopo Mbezi eneo la Goba jijini Dar es Salaam
Yeremiah Mbaga Katibu wa Kundi hilo amesema kuwa kuna kila sababu kwa jamii, wazazi na walezi kuishi vema na kujiweka kando na migogoro ya kifamilia ili kuepusha kusambaratika kwa familia .
“Tusifike pahala mtoto kulelewa kwenye taasisi ikiwa wazazi wapo mtoto alelewe humu ikiwa hakuna budi”, alisema Mbaga.
“Kitu ambacho kimetugusa ni sababu zinazowafanya watoto waje kulelewa hapa ni sababu za kusikitisha kwa sababu inaonekana jamii imeacha mungu imepotoka kwa sababu ya vituko na madhila ambayo watoto hawa wamepitia” amesema Mbaga.
Mbaga amesisitiza watu kutoacha misingi ya sheria za nchi na kufuata maamrisho ya Mungu pamoja na kuacha kuiga mila za kigeni.
Naye, Lucas Kaigarula mmoja wa wanachama wa kundi hilo amesema kuwa kundi hilo limewakutanisha wastaafu mbalimbali waliokuwa wanafanyakazi TRA.
“Kundi hili liliundwa ili kuleta umoja miongoni mwetu lakini kuzidisha upendo na kushirikiana ” amesema Kaigarula.
Amesema kuwa umoja huo uliimarishwa tarehe 1 Desemba 2024 walipofanya sherehe iliyowakutanisha pamoja ‘Get Together’ .
Amesema wameamua kutoa msaada kwenye kituo hicho ili kumpendeza mungu lakini pia kuwapa moyo watoto hao wasijione kuwa wako peke yao bali jamii nzima inawapenda na kuwatambua.
Kerina Misso, Mweka Hazina wa kundi hilo amesema kuwa dhamira ya kundi hilo kukutana pamoja pia kuisaidia jamii.
Amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wazazi kushindwa kuwalea watoto na kuwafanya kuishi katika mazingira magumu hamaye kulelewa na taasisi.
“Sisi wazazi tumeacha majukumu yetu ya kulea watoto wetu tumeziachia taasisi naomba nitoe wito kwa wazazi wote kama waliteleza sisi sote binaadamu tunateleza lakini turudi kwenye mstari tukumbuke kwamba ni jukumu letu kuhakikisha hawa watoto wanakuwa kiafya na kimaadili”, amesema Misso.
Kwa upande wake Gerald Soka Mlezi wa kituo cha Watoto Wetu amewashukuru wastaafu wa TRA kwa kuwakumbuka watoto hao.
Amesema kuwa kituo hicho kinalea watoto zaidi ya 75 hicho wenye umri wa kusoma shule ya awali hadi shule ya msingi .
Soka amesema kuwa kituo hicho kimefanikiwa kulea watoto mpaka kuhitimu watoto sita ngazi ya shahada ya uzamili watoto watoto 42 ngazi ya shahada ya awali .
Amezitaja changamoto zinawakabili ikiwa pamoja na changamoto ya kisaikolojia inayowakumba watoto kutokana na ukatili waliofanyiwa na walezi mpaka kufikia kulelewa hapo.
Amesema kuwa Changamoto nyingine ni pamoja na ukosefu wa ada kwa watoto wanaosoma katika shule mbalimbali .