NA BELINDA JOSEPH, MWANZA.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Silas Isangi, amesema kuwa maboresho yaliyofanywa katika katiba ya RT ya mwaka 2020 yalikuwa muhimu na yanajumuisha masuala ya elimu, umri wa viongozi, muda wa kukaa madarakani, na vigezo vya kupiga kura kwa wajumbe kutoka kila mkoa. Isangi alisema, “Mpiga kura kutoka kila mkoa atakuwa ni mwenyekiti, na ibara zote zilizokuwa hazijakaa sawa zimeboreshwa.”
Mkutano maalumu wa marekebisho ya katiba ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) umefanyika Februari 28, 2025, jijini Mwanza. Mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali wa michezo na viongozi wa riadha kutoka mikoa zaidi ya 20 ya Tanzania Bara, ambapo lengo kuu lilikuwa kujadili na kufanya maboresho ya katiba na kanuni zinazohusiana na usimamizi wa mchezo wa riadha nchini.
Aidha, Rais Isangi alieleza kuwa katiba mpya imepitishwa kwa umoja na kwamba imeridhiwa na kila mjumbe. “Katiba imepita vizuri, wataifurahia wadau wa michezo, na itakuwa nzuri,” alisema.
Akizungumzia uhaba wa viwanja vya michezo, Isangi amesema kuwa serikali inaendelea kujikita katika ujenzi wa viwanja vya riadha vitakavyosaidia kukuza mchezo huo , Aliongeza kuwa mikoa ambayo bado haina viwanja bora itatumia viwanja vilivyopo kuendeleza michezo ya riadha, huku akisisitiza kuwa wanariadha wanahitaji miundombinu bora ili kuwakilisha Tanzania kimataifa.
Rais Isangi ametoa rai kwa wenyeviti wa mikoa kuendelea kushirikiana na wanariadha ili kuboresha michezo hiyo. Amesema kuwa, sasa baada ya maboresho ya katiba, viongozi wa RT wataweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar, Muhidin Kasunzu, amempogeza Rais wa RT kutokana na mabadiliko hayo kwani anasema yatakwenda kuleta chachu ya mchezo huo na kutoa nafasi kwa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika mashindano. Kasunzu ana matumaini kuwa mabadiliko haya yataufikisha mchezo huo kimataifa.
Christina Paga, mjumbe kutoka Simiyu, amesema kuwa maboresho ya katiba yamewapa nguvu wanawake, kwani wamepiga hatua kubwa katika kutambua nafasi yao kwenye Shirikisho la Riadha. Alitoa rai kwa wanawake kuwa na mwamko wa kuwania uongozi kwani katiba inatoa nafasi kwao kuongoza nyadhifa mbalimbali.
Mchakato wa maboresho ya katiba ya RT ulianza miaka kadhaa iliyopita na hatimaye umetamatika Februari 28, 2025. Kamati huru ilianzishwa na RT ili kuandaa rasimu ya mabadiliko, ambayo ililenga kuboresha maslahi ya mchezo wa riadha. Safari ya maboresho hayo imehitimishwa jijini Mwanza, ambapo wajumbe kutoka mikoa mbalimbali waliridhia kwa umoja na kupitisha maboresho hayo rasmi.