Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao baadaye ulifuatiwa na semina fupi kwa wajasiriali hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Benki ya CRDB, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Exaud Kagahe alisema “Serikali inajua faida za mkataba huu ndiyo maana Bunge liliidhinisha mnamo Septemba 2021, na hivyo kuifanya nchi yetu kustahiki kunufaika na Soko Huria la Afrika. Uamuzi huu wa serikali unalenga kufungua fursa kwa wajasiriamali wetu nje ya mipaka yetu ya kitaifa,”
Aliendelea kusema “Ili kuchukua fursa hizi kikamilifu, watu wetu lazima wawe na taarifa sahihi, maarifa muhimu, na ujasiri wa kuvuka mipaka kutafuta fursa hizi popote zinapojitokeza ndani ya mataifa 55 yetu Bara la Afrika. Kinachoendelea katika semina ya leo ni sehemu ya mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali wetu kushindana na wenzao sokoni.”
Akielezea jukumu la CRDB Bank katika programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, TullyEsther Mwambapa alisema taasisi yake imejipanga kuhakikisha inatoa elimu ya fedha, mafunzo ya biashara na mitaji wezeshi itakayo wawezesha wajasiriamali kunufaika na Soko Huria la Afrika (AfCTA) linalokadiriwa kuwa na watu zaidi ya bilioni 1.4.
Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mkurugenzi Mkaazi wa Shrika hilo, Shigeki Komatsubara alieleza fursa zinazoambatana na soko huru la AfCTA ikiwamo kuongezeka kwa biashara za ndani, kuvutia uwekezaji, na kuchochea mabadiliko ya kiuchumi hasa kwa wanawake wajasiriamali kote barani Afrika.



