Wakati Dunia ikielekea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2025, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya ALAF wametoa vifaa mbalimbali muhimu kwa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya zoezi la utoaji wa vifaa hospitalini hapo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya ALAF, Bi Hawa Bayumi alisema mpango huo ni wa wafanyakazi wanawake wote ambao walichangia kutoka mifukoni mwao kwa ajili ya mpango huo na kupata muda wa kujumuika na baadhi ya wagonjwa katika wodi ya wazazi.
“Mpango huu, ambao ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, unaendana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira safi na salama kwa akina mama na watoto hospitalini, kuimarisha afya na ustawi wao,” alisisitiza.
Aidha, alisema kwamba mchango wao huo unaonyesha moja kwa moja kujitolea kwao kwa maadili ya msingi ya kutoa huduma na ubia wa kampuni.
Kulingana na Bi Hawa, ishara hii inalingana na dhamira ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ya mwaka 2025, “Harakisha Kuchukua Hatua,” inayoonyesha umuhimu wa hatua za haraka na zenye matokeo ya kusaidia afya, usalama na uwezeshaji wa wanawake.
Kwa upande wake, Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya ALAF Jumbe Onjero aliwapongeza wafanyakazi wanawake kwa kuwajali wanawake wenzao wanaohitaji msaada ili kuhakikisha wanajifungua salama.
“Kwa kutoa vifaa hivi muhimu vya usafi, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya ALAF wanalenga kuleta matokeo ya maana na yanayoonekana katika jamii, kusherehekea nguvu na ujasiri wa wanawake,” alisema Meneja wa Rasilimali Watu.
Alisema kupitia juhudi hizi na nyinginezo, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya ALAF wanashiriki kikamilifu katika kuchangia harakati za kimataifa za maendeleo ya wanawake.
Wakati huo huo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Bi Grace Samson Wella, aliwashukuru wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya ALAF kwa ukarimu huo na kusema msaada huo utawasaidia sana wanawake wakati wa kujifungua, hasa wale wasio na uwezo kifedha wa kumudu vifaa hivyo.
“Tunatoa wito kwa wanawake wengine kuiga kile ambacho wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya ALAF wamefanya na nina hakika tutaokoa maisha mengi huko nje,” alisema.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kutengeneza vifaa vya chuma vya kuezekea majengo.
Baada ya kuanzishwa mwaka 1960, imekukuwa muda wote mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Kampuni ya ALAF si tu huzalisha vifaa vya kuezekea vya chuma, lakini pia vifaa vingine mbalimbali vya ujenzi na mabomba kwa matumizi mbalimbali.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi
(kulia), akimkabidhi mmoja wa wazazi waliojifungua, Asha Salum, wakati
wafanyakazi wanawake wa kiwanda hicho walipoenda kutoa msaada
kwenye Wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa yaTemeke Dar
es Salaam Jumanne. Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited Hawa Bayumi
(kulia), akikabidhi baadhi ya vitu mbalimbali vilivyotolewa na kiwanda
hicho, kwa Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Rufaa ya
Temeke, Grace Wellia, kwa ajili ya wazazi waliojifungua katika
hospitali hiyo jijini Dar es Salaam
Afisa Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Theresia Mmasy (katikati), akimkabidhi vifaa mbalimbali mmoja wa wazazi waliojifungua Sarah Kamani,
wakati wafanyakazi wanawake wa kiwanda hicho walipoenda kutoa
msaada kwenye Wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa
Temeke Dar es Salaam Jumanne