Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, wanawake kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imejitolea kugharamia matibabu ya kiasi cha TZS milioni mbili na nusu kwa watoto wanaougua saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na msaada wa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya TZS 710,000 ikilenga kuboresha huduma za matibabu kwa watoto hao na kupunguza changamoto zinazowakabil.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Grace Kiunsi, mnamo tarehe 05 Machi, 2025 alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya mchango wa TCAA katika kusaidia jamii, hususan sekta ya afya, akisisitiza kuwa wanatambua changamoto wanazokutana nazo watoto na familia zao wanaopokea matibabu ya saratani.
“TCAA inajivunia kushiriki katika kuboresha huduma za matibabu kwa watoto hawa. Tunaamini msaada wetu utasaidia kuboresha utoaji wa dawa kwa wakati na kupunguza mzigo kwa wazazi ambao mara nyingi wanakutana na changamoto kubwa ya kugharamia matibabu ya watoto wao,” alisema Kiunsi.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Afisa Muuguzi na Kiongozi wa Wodi ya Watoto, Maria Myula, alisema kuwa msaada huo ni muhimu katika kuhakikisha hospitali inaendelea kutoa huduma bora kwa watoto wenye saratani, hususan wale wanaotegemea msaada wa serikali na wadau wengine wa afya.
“Tunashukuru TCAA kwa msaada huu wa kipekee. Saratani ni ugonjwa unaohitaji rasilimali nyingi, na msaada huu utasaidia kununua dawa muhimu, vifaa tiba, na maboresho ya mazingira ya matibabu ili kuwapa watoto wetu nafasi nzuri ya kupona,” alisema Myula.
MNH ina kitengo maalum kinachoshughulikia matibabu ya watoto wenye saratani ambapo serikali imewekeza katika matibabu ya saratani za mifupa, ini, figo, misuli, tishu, ubongo, matezi, pamoja na saratani ya damu, ambazo zinahitaji matibabu maalum na ya gharama kubwa.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Grace Kiunsi akikabidhi baadhi ya mahitaji kwa wawakilishi wa wazazi wa watoto watoto wanaougua saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Grace Kiunsi akitoa neno kwa wazazi wakati wa kukabidhi mahitaji kwa wawakilishi wa wazazi wa watoto watoto wanaougua saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Muuguzi Mkunga Kitengo cha magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akitoa elimu kuhusu ugonjwa wa saratani kwa baadhi ya wanawake kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) waliofika kukabidhi mahitaji kwa watoto watoto wanaougua saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Baadhi ya wanawake kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) waliofika kukabidhi mahitaji kwa watoto watoto wanaougua saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Picha ya pamoja