Na Jane Edward, Arusha
Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dkt Stagomena Tax amewaasa wanawake wote nchini kuhakikisha wanalinda haki na ustawi wa jinsia zote ili kuwa na Taifa lenye usawa.
Dkt Stagomena ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika kongamano la wanawake kanda ya Kaskazini kuelekea siku ya wanawake duniani 2025 lililofanyika jijini Arusha.
Amesema kuwa zipo changamoto kwa pande zote na sio kwa watoto ambapo kumekuwepo na changamoto ya ukosefu wa fursa sawa za kiuchumi ambayo hupelekea wao kufanya kazi kwenye mazingira ya chini.
Aidha amewataka wanawake kuzitumia ipasavyo fursa za kiuchumi pindi wanapopewa fursa hizo wahakikishe wanazitendea haki kama ambavyo Rais Samia anavyofanya ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake.
Amesema,anataka kuona wanawake wananufaika ipasavyo na fursa mbalimbali za kiuchumi pamoja na kuchangamkia nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi mbalimbali kwani wana mchango mkubwa sana katika jamii.
Kwa upande wake Naibu waziri wizara ya maendeleo ya jamii ,jinsia ,wanawake na makundi maalum Mwanaidi Ally Hamis amesema katika kongamano hilo wataweza kujadili mchango wa sekta ya maliasili na utalii kwa wanawake kwani wanawake sasa hivi wamekuwa mstari wa mbele katika kumuunga Rais Samia mkono kwenye swala ya utalii.
Aidha amewataka wanawake kuhakikisha wanalinda jamii zetu sambamba na kutenga muda kwa ajili ya watoto wetu kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaisha kabisa.
Katika kongamano hilo Tafiti 16 zitajadiiwa ambazo zinalenga kuwajengea uwezo wanawake katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya uongozi utalii na fursa zilizopo .