
Tarehe 7 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Askofu Stephano Lameck Musomba OSA kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, lililoundwa kwa kuligawa kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro, kwa mujibu wa taarifa kutoka Vatican.
Kanisa Kuu la Jimbo hili ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, mjini Bagamoyo, lina Parokia 22, Mapadre wa Jimbo 8, Mapadre Watawa 37 na Watawa 8.
Askofu Musomba alizaliwa tarehe 25 Septemba 1969, kijijini Malonji, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe. Wazazi wake ni Lameck Musomba na Maria Kandonga.
Alisoma Shule ya Msingi Malonji (1979-1985), kisha Seminari Ndogo ya Maua (1989-1995). Baadaye, alisoma Falsafa na Taalimungu katika Taasisi ya Wasalvatoriani, Morogoro (1995-2003).
Safari yake ya kitawa ilianza 1988, akiwa Shirika la Waagustiniani (OSA). Aliweka Nadhiri za Daima tarehe 25 Septemba 2002, na mwaka huo huo, alipata Daraja ya Ushemasi. Tarehe 24 Julai 2003, akapewa Daraja Takatifu ya Upadri huko Mahanje, Songea.
Alianza kuhudumu kama Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mavurunza (2003-2004). Kisha alisomea Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology) huko Roma, Italia (2004-2008), akipata Shahada ya Uzamili ya Taalimungu.
Amewahi kuwa Paroko wa Temboni (2009-2015), Mlezi wa Shirika la Waagustiniani Morogoro (2016-2019) na Katibu Mwakilishi wa Waagustiniani Tanzania (2008-2021).
Tarehe 7 Julai 2021, Papa Francisko alimteua kuwa Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam, akapewa daraja la uaskofu 21 Septemba 2021.
#makinikiyayahabari
#AskofuStephanoLameckMusombaOSA
#jimbokatolikibagamoyo