KATIKA maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 08, 2025 Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetoa wito kwa jamii, vyama vya siasa, na vyombo vya habari kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa haki kwa wagombea wa jinsia zote, hasa wanawake.
TAMWA imeeleza kuwa uchaguzi wa mwaka huu unaashiria hatua kubwa kwa ushiriki wa wanawake katika uongozi, huku wagombea wawili wa kike – Rais Samia Suluhu Hassan (CCM) na Dorothy Semu (ACT-Wazalendo) – wakipambana kuwania nafasi ya juu kabisa nchini. Hata hivyo, chama hicho kimeonya kuwa bado kuna changamoto kubwa, ikiwemo udhalilishaji wa wanawake kwenye kampeni na mitandao ya kijamii, hali inayoweza kuzuia ushiriki wao kikamilifu.
Kwa mujibu wa UN Women, idadi ya wanawake katika uongozi wa juu bado ni ndogo, huku dunia ikikadiriwa kuchukua zaidi ya miaka 130 kuziba pengo la kijinsia katika siasa. Tanzania pia bado ina uwakilishi mdogo wa wanawake katika nafasi za uongozi:
Wabunge wanawake wa kuchaguliwa: 9.1%
Wabunge wa viti maalum: 29%
Madiwani wa kuchaguliwa: 3.8%
Madiwani wa viti maalum: 26.2%
Kwa kuzingatia hali hii, TAMWA imetoa mapendekezo maalum kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu hauzuii wanawake kushiriki ipasavyo:
Kampeni za heshima: Lugha ya matusi na dharau dhidi ya wagombea wanawake izuiwe.
Vyama vya siasa viwape nafasi wanawake: Wanawake waaminiwe kugombea majimbo badala ya kutegemea viti maalum pekee.
Kuhukumu sera, si maisha binafsi: Maisha ya mgombea (ndoa, watoto, sura) yasitumiwe kama hoja za kisiasa.
Usawa kwenye vyombo vya habari: Habari ziwe za haki kwa wagombea wa jinsia zote, bila ubaguzi au maudhui ya udhalilishaji.
Mitandao ya kijamii itumike vizuri: Jamii isambaze ujumbe wa kuhamasisha usawa, si chuki na kejeli kwa wanawake wanaogombea.
TAMWA imesisitiza kuwa uchaguzi wa haki utahakikisha wanawake wanapata fursa sawa kushiriki siasa bila hofu. Wito umetolewa kwa taasisi zote kuungana katika kuhakikisha Tanzania inafanya uchaguzi wa kidemokrasia unaojali usawa wa kijinsia.