MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameliomba Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) kumwombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na taifa zima kwa ujumla hasa wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu.
Mpogolo, ameyasema hayo, alimpomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika ibada ya maalumu ya kumsimika Askofu Jackson Malongo, kuwa Askofu Mkuu Jimbo la Pwani la Kanisa hilo.
“Tuendeleee kuliombea taifa letu. Tumuombee Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na yeye ndiyo kiunganishi kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani,”amesema.
Ameeleza, Rais Dk. Samia, ndiye mama na mlezi ambaye amesimama imara kuhakikisha taifa linasonga mbele.
Mpogolo amesemakatika Wilaya ya Ilala pekee Rais Dk. Samia ametoa sh. bilioni 317 za maendeleo ambazo zitamaliza changamoto mbalimba zikiwemo za maji na barabara.
“Tuwaombee watanzania wote, amani na mshikamano. Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi Mkuu. Tuweke taifa letu kwenye sala zetu. Tumalize uchaguzi kwa amani na utulivu,”amesema Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha amewataka waumini wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kujiandikisha na kuhuisha taarifa zao katika Dafrtari la Kudumu la Wapigakura.
“ Tuwaambie na tuwahamasishe watoto wetu kwenda kujiandikisha. Wale waliojiandikisha waende kuhakiki taarifa zao,”amesema.
Amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kanisa hilo na kumpongeza Askofu Malongo kuwa Askofu Mkuu Jimbo la Pwani.
“Nakushkuru Makamu Askofu Mkuu na Askofu Mkuu kwa kuridhia kumwalika Mkuu wa Mkoa katika ibada hii muhimu.Heshima hii hatuta iweka chini bali tutaiweka juu,”amebainisha.
Awali, Askofu Mkuu wa Jimbo la Pwani la FPCT, Malongo, alisema kanisa mama la makanisa hayo limekuwepo nchini tangu mwaka 1932.
Alisema kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwake hapa nchini kwa uongozi wa Wamisionari na baadaye wazawa limekuwa na ushirikiano mkubwa na serikali ya Tanzania.