NA VICTOR MASANGU,PWANI
TAASISI ya Lions Club imegawa msaada wa futari pamoja na mahitaji ya vyakula mbali mbali kwa kwa wananchi kutoka katika Vijiji kumi vilivyopo kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagsmoyo Mkoa wa Pwani.
Msaada huo ambao umetolewa umewalenga hasa makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ikiwa pamoja na wazee mbali mbali wanaoishi katika kata hiyo ya Vigwaza.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa misaada hiyo Mwenyekiti Mstaafu wa Lions Club Muntazir Bharwani akiongozana na Mwenyekiti wa sasa Mahmood Rajuani na Shahid Mitha wamesema kwamba wamegawa msaada huo kwa wananchi zaidi ya 70 ambapo wametumia zaidi ya shilingi milioni tatu katika kununua mahitaji hayo.
Akizungumza baada ya hafla hiyo Muntazir amesema hadi sasa wamefikia vituo Saba ambavyo tayari wamegawa vyakula na futari tangu mwezi wa Ramadhani ulipoanza.
Amesema lengo lao ni kufikia katika vituo 20 kabla mwezi wa Ramadhani kuisha ambapo wanufaika watapatiwa vyakula na futari vitakavyowasaidia katika kipindi cha mfungo.
” Vyakula hivi na misaada tunayotoa ni michango ya wafadhili kutoka maeneo mbalimbali ambao wanaguswa na tunachofanya kuwafikia wahitaji tutaendelea kufanya ibada hii ya kutoa sadaka kadiri ya tutakavyochangiwa,” amesema.
Mwenyekiti mstaafu huyo amesema pamoja na kuwa ofisi yao ipo Mkoa wa Dar es Salam wamelazimika misaada yao kupeleka maeneo ya nje ya mkoa huo ambayo hayafikiwi kwa urahisi pamoja na kuwa wahitaji wengi wako huko.
Hadi sasa Lions Club imefikia eneo la Pugu, Kimbiji, Gongolamboto Mkuranga, Vikindu, Mbande na sasa Vigwaza ambapo mbali ya kutoa vuakula na furari pia walitoa misahafu, Juzuu na gypsum board kwa ajili ya msikiti uliopo Ruvu.
Diwani wa kata hiyo Mussa Gama ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwezesha vuakula hivyo kwa wazee na watu wenye mahitaji huku akiwaomba wadau wengine wenye uwezo kukumbuka kusaidia makundi hayo.
Zakia Ally mkazi wa Kitonga na Editha Michael ni kati ya wanufaika wa msaada huo ambao wameishukuru Taasisi hiyo pamoja na Diwani aliyewaunganisha kufikia na misaada hiyo.



