Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Ludewa sambamba na kamati ya Ushauri wilaya limepitisha azimio la kugawa Jimbo la Ludewa na kuwa majimbo mawili ya uchaguzi ili kuweza kusogeza huduma kwa wananchi kwa urahisi zaidi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mnamo Februari 2,2025 Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi kutoa tangazo la kuruhusu mchakato wa kugawa ama kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi huku katika hatua ya ugawaji majimbo ikiweka vigezo vya idadi ya watu kuanzia 600,000 kwa mijini na 400,000 kwa vijijini.
Vigezo vingine ni ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, hali ya kiuchumi ya jimbo, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya ama halmashauri mbili, mpangilio wa makazi ya watu, idadi ya wabunge viti maalum wanawake, uwezo wa ukumbi wa bunge, upatikanaji wa njia za mawasiliano pamoja na hali ya kijiografia ya eneo husika.
Awali akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya ugawaji wa jimbo hilo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mathan Chalamila amesema sababu ya kuomba kuligawa jimbo hilo ni kutokana na Halmashauri hiyo kuwa na jumla ya eneo la kilometa za mraba 8,397 kwa maeneo ya ardhi na maji ambapo eneo la ardhi ni KM. 6,325 na majini ni 2,072 hivyo ukubwa huo umekuwa umekuwa ukiathiri utoaji huduma kwa wananchi kwani muda mwingi na gharama kubwa zimekuwa zikitumika katika kufikisha huduma.
Aidha ameongeza kuwa katika suala la ukuaji wa uchumi limekuwa likisuasua kutokana na mazingira ya kijiografia yanayopelekea vijana kukimbilia mijini na kuwaacha wazee huku idadi ya watu kwa sensa ya mwaka 2022 ikionyesha kuwa na jumla ya watu 151,361 ikiwa ni ongezeko la watu 18,143 kwa sensa mwaka 2012.
Hata hivyo katika hali ya mawasiliano Kaimu Mkurugenzi amesema kuwa maeneo yote ya wilaya hiyo yanafikika na mitandao ya Mawasiliano ya simu huku maeneo ya Tarafa ya Mlangali,.Masasi, Liganga, na Mawengi yanafikika kwa njia ya barabara wakati wote na eneo la Tarafa ya Mwambao ikifikika kwa majini.
Sanjali na hayo lakini pia ugawaji wa majimbo hayo umezingatia mipaka ya kiutawala ambapo jimbo la Ludewa Kaskazini litakuwa na Tarafa mbili ambazo ni Tarafa ya Liganga na Mlangali huku Jimbo la Ludewa Kusini likiundwa na Tarafa tatu ambazo ni Tarafa ya Mawengi, Masasi na Mwambao.