
BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali(NaCoNGO), limezindua kikosi kazi cha kitaifa chenye wajumbe 14 wanaotoka katika makundi ya wawakilishi mbalimbali kwa ajili ya kukusanya maoni ya wadau pamoja na kufanya mapitio ya kanuni zinazosimamiwa na baraza hilo.
Akizindua Kikosi hicho mapema leo Machi 12,2025 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Baraza hilo,Gasper Makala amesema kikosi kazi hicho cha wajumbe kitafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Kampuni ya Will Global ambao ni Henry Muguzina na kusaidiwa na Bubezwa kaiza.
Akitaja majina ya wajumbe wa kikosi kazi hicho ambao wataongozwa na yeye Makala wengine niAdamson Nsimba ambaye ni Katibu Mkuu, NaCoNGO ,Prisca Ngweshemi ,Muweka Hazina wa NaCoNGO ,Joram Hongoli Mjumbe wa NaCoNGO ,Patrice Gwasma Mjumbe wa NaCoNGO ,Edison Mwakyembe Mjumbe wa NaCoNGO .
Wengine ni Lupi Mwaisaka nambaye ni Mjumbe wa NaCoNGO, Francisca Damian Mjumbe wa NaCoNGO Vijana , Advocate Mariam Othman ambaye ni Mkurugenzi Mtendeni TLS, Dkt.Riziki Nyello Mhadhiri Institute of Social Work,Dkt.Astronaut Bagile Mkurugenzi Kampuni ya WISE, Advocate Gloria Mafole kutoka CCT, Asina Shenduli kutoka Baraza la Waislamu Tanzania( BAKWATA ) pamoja na Edmund Matotay kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Amesema kazi ya kamati hiyo ni kukusanya maoni ya wadau mbalimbali na kuhakikisha chochote kitakachokusanywa kinakuwa shirikishi na kuwa na ladha ya wanasekta ya NGo’s.
“Mchakato huu wa kukusanya maoni kutoka wadau umewezeshwa na Ubalozi wa Mataifa(EU) ikiwemo kupitia kanuni zinazosimamiwa na baraza hilo,”amesema.
Aidha aliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa ushirikiano mkubwa tangu Baraza jipya lilipoingia madarakani.
”Ikumbukwe kwamba Agost 28,2024 tuliwajulisha waandishi wa habari kuanza kwa zoezi hili,ambapo Februari 21,2025 tuliwatangazia umma kuwa leo ndio itakuwa siku rasmi ya kuzindua zoezi hili la ukusanyaji wa maoni chini ya kikosi kazi hicho.
“Tutafanya mapitio ya kanuni zinazosimamia na baraza hilo za Mwaka 2016 ,tutafanya mapitio ya kanuni za uchaguzi wa baraza za NaCoNGO za Mwaka 2016 na tutafanya mapitio ya mkakati wa mpito ya baraza hilo ili kuboresha mkakati mpitio,”amesema.
Kwa upande Meneja wa Asasi za Kiraia kutoka Umoja wa Ulaya(EU),Neema Bwaira amesema Umoja wa ulaya ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini Tanzania kwani wanafanya kazi na waadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Asasi za Kiraia.
Amesema kupitia zoezi hilo linalofanywa na Baraza la NaCoNGO wameona kuna umuhimu wa kushirikiana na kufanya kazi na baraza hilo ili kuweza kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Asasi za Kiraia Tanzania.
”Sisi kama wadau maendeleo tunawatakia mchakato mwema ambao utakwenda kukusanya maoni na kupitia kanuni kama zilivyoainishwa pamoja na kuuisha Mpango mkakati wa NaCoNGO utakaoweza kuhakisi mambo mbalimbali,”amesema.
Aidha amesema anaamini kuwa kazi yote itakayofanyika itakuwa kwa manufaa ya sekta za Asasi ya kiraia Tanzania na maendeleo ya nchi ya Tanzania na wananchi kwa ujumla.