Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 11 Machi, 2025 limetoa magodoro zaidi ya 300 katika kuunga mkono Kampeni ya Achia Gheto Hamia Hosteli inayolenga kuchagiza wanafunzi wa wilaya Kisarawe kuhamia shule zenye hosteli kwa lengo la kuongeza ufaulu wa masomo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema TASAC imeguswa na kampeni hiyo iliyoanzishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Petro Magoti, ambaye anahimiza wanafunzi kukaa mashuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu na si kukaa katika nyumba za kupanga au kutokea majumbani hali inayosababisha kushusha ufaulu wa wanafunzi hao.
Bw. Salum ameongeza kuwa TASAC kupitia Sera ya Kurejesha kwa Jamii imeamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais ambaye amelenga kuongeza ufaulu katika elimu ya sekondari hasa kwa wanafunzi wa jinsia ya kike.
“Sisi kama taasisi ya umma tunashiriki katika kampeni hii kwa lengo la kumuunga mkono kwa vitendo Mheshimiwa Rais, kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa bora ya kusoma ili kuongeza ufaulu wa masomo hasa kwa wanafunzi kike ambao hawaishi mashuleni,” amesema Bw. Salum.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Mhe.Petro Magoti ameishukuru TASAC kwa kuwezesha kampeni hiyo kwa kutoa msaada ambao utaongeza idadi kubwa ya wanafunzi kuhamia katika shule zenye hosteli zilizopo wilayani humo.
“Hakika msaada huu utasaidia wanafunzi wengi wa madarasa yenye mitihani, yaani wa kidato cha pili na kidato cha nne kuweza kuhamia hosteli ambapo tumelenga kuwaweka pamoja kwa lengo la kuongeza ufaulu wilayani Kisarawe,” amesema Mhe. Magoti.
Aidha, Mhe. Magoti ameagiza wenye nyumba watakaokutwa wamewapangisha wanafunzi wa vidato hivyo, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa awamu hii, magodoro hayo yametolewa kwa Shule za Sekondari Chole, Kurui, Kibuta, Kisangire, Mfulu na Mzenga.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) Mohamed Salum akikabidhi msaada wa magodoro zaidi ya 300 katika kuunga mkono Kampeni ya Achia Gheto Hamia Hosteli inayolenga kuchagiza wanafunzi wa wilaya Kisarawe kuhamia shule zenye hosteli kwa lengo la kuongeza ufaulu wa masomo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) Mohamed Salum akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti wakati TASAC ilipokwenda kukabidhi msaada wa magodoro zaidi ya 300 katika kuunga mkono Kampeni ya Achia Gheto Hamia Hosteli inayolenga kuchagiza wanafunzi wa wilaya Kisarawe kuhamia shule zenye hosteli kwa lengo la kuongeza ufaulu wa masomo.
Picha katika makundi mbalimbali mara baada ya kukabidhi msaada wa magodoro zaidi ya 300 katika kuunga mkono Kampeni ya Achia Gheto Hamia Hosteli inayolenga kuchagiza wanafunzi wa wilaya Kisarawe kuhamia shule zenye hosteli kwa lengo la kuongeza ufaulu wa masomo.