Na Mwandishi Wetu,
DODOMA, 12 Machi, 2025
SERIKALI imelieleza Bunge kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika utafutaji wa fedha kwa ajili ya kuongeza idadi na tija ya utekelezaji wa miradi inayohusu hifadhi ya mazingira nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akiwasilisha taarifa kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya maji na mazingira kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa mwaka 2024/2025.
Mhe. Khamis amesema lengo la miradi ya hifadhi ya mazingira iliyopo nchini ni kuhakikisha Ofisi ya Makamu wa Rais inachangia kikamilifu katika mpango wa maendeleo wa taifa na ukuaji wa uchumi endelevu.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2024/2025 miradi ya maendeleo ya hifadhi ya mazingira inayotekelezwa na kusimamiwa na Ofisi hiyo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa kuta katika fukwe za Mikindani- Mtwara na Sipwese- Pemba, Mradi wa kuboresha eneo la bwawa la kuhifadhi maji ya mvua la Swaswa-Mnarani.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania (LDFS), Mradi wa usimamizi Jumuishi wa Mifumo ikolojia, Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayonuai Tanzania (SLR).
Naibu Waziri Khamis ameitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na Mradi wa kuandaa Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa kuhifadhi Bayonuai, Mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBBAR) na Mradi wa kujenga Ustahimilivu wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi uliopo Mkoani Kigoma.
Amesema kupitia miradi hiyo, jamii zimewezesha utekelezaji wa shughuli mbadala za kiuchumi na rafiki kwa mazingira ikiwemo mipango ya kisasa ya ufugaji endelevu, uendelezaji wa mashamba darasa ya malisho, ujenzi wa skimu za umwagiliaji na mipango ya kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Mhe. Khamis amelieleza Bunge kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tanzania Bara na Zanzibar) na imeongeza tija katika ukuaji wa maisha na ustawi wa huduma za kijamii na kiuchumi kupitia uhifadhi endelevu wa mazingira.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zimeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira nchini.
“Tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa kutokata miti ovyo ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na tumeendelea kuhamasisha sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika na taasisi za umma kuunga mkono jitihada hizi” amesema Mhe. Khamis.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga Mkoani Iiringa, Mhe. Jackson Kiswaga ameipongeza ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kuwa kamati hiyo itajifunza masuala mengi zaidi wakati wa ziara inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Kamati hiyo inatarajia kuanza ziara ya kutembelea miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwemo Mradi Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika maeneo kame ya Tanzania (LDFS), Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayonuai Tanzania (SLR-Tanzania).
Mradi mwingine ni pamoja na mradi wa Mradi wa kujenga Ustahimilivu wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi uliopo Mkoani Kigoma.
(NA MPIGAPICHA WETU)