-Wadau wapongeza uwepo wa ubao wa kidigitali wa kuonesha bei elekezi za madini
Wadau wa madini wakiwemo wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini katika mkoa wa Shinyanga wamepongeza uwepo wa Soko la Madini-Shinyanga, ambalo tangu kuanzishwa kwake limekuwa msaada mkubwa ambapo madini yanauzwa kulingana na bei elekezi inayoendana na soko la dunia ambayo huoneshwa kwenye ubao maalum wa kidigitali.
Akizungumza leo Machi 12, 2025 katika soko hilo, Afisa kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Shikimayi Muyinza amesema, soko hilo limekuwa na tija kubwa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini mkoani humo ambapo Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa bei elekezi na kuepusha changamoto za wachimbaji kupunjwa kwa kupewa bei ndogo na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.
“Ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma, Soko hili linatumia ubao unaotumia teknolojia ya kidigitali ambao unaonyesha bei elekezi za madini ya dhahabu sambamba na madini mengine kama vile shaba na fedha ili kuongeza uwazi kwenye shughuli za biashara hapa sokoni tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo bei elekezi iliyokuwa inatolewa ni ile ya madini ghafi ya dhahabu tu ”amesema Muyinza.
Aidha, baadhi ya wadau wa madini mkoani Shinyanga wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini kwa hatua ya uanzishwaji na usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini kwani yameleta mabadiliko ya kiuchumi katika Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni pamoja na ajira, mapato kwa Serikali na kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za uchimbaji wa madini katika mkoa huo.