Na. Peter Haule, WF, Rorya Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka, ametoa agizo kwa taasisi zenye tabia ya kushikilia kadi za benki za watumishi wa Umma kama dhamana wanapokopa kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume cha Sheria.
Agizo hilo amelitoa Wilayani Rorya alipotembelewa na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha ikiongozwa na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, iliyofika kwa ajili ya kutoa elimu katika Wilaya hiyo.
Bw. Mtaka alisema kuwa ameandaa Timu inayo kusanya taarifa ya vitendo hivyo na baada ya kukamilika hatua mbalimbali zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
“Wapo watumishi ambao wanakopa katika Sekta rasmi zikiwemo Benki kwa kuzingatia utaratibu wa kiasi kinachotakiwa kusalia katika mishahara yao na baada ya hapo wanakwenda kukopa kwenye taasisi zisizo rasmi ambazo huchukua Kadi zao za Benki na namba za Siri na kuchukua fedha zinazoingia ili kurejesha mkopo”, alisema Bw. Mtaka.
Alisema kuwa tatizo hilo linawafanya watumishi kutofanya kazi kwa ufanisi kwa kuwa wanajikuta hawana fedha za kukidhi mahitaji yao ya muhimu.
Bw. Mtaka alisema kuwa kitendo cha kukopa kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria kwa mtumishi ni kosa lakini pia taasisi zinazotumia mwanya huo kutenda vitendo viovu kwa watumishi nalo ni jambo lisilokubalika, kwa hiyo atachukua hatua stahiki mara baada ya zoezi hilo la wataalamu wake kukamilisha jukumu alilowapa.
Alieleza kuwa kwenye utumishi wa umma kuna miongozo na Kanuni zinazomuelekeza mtumishi namna ya kukopa na akienda kinyume Kanuni zimeelekeza hatua za kumchukulia.
Alitoa wito kwa watumishi ambao hawazingatii miongozo hiyo ambao wamekopa Benki na taasisi nyingine nje ya Benki na mwajili hajahusishwa kwenye makubaliano na wamekopa zaidi ya wanavyoruhusiwa kukopa waache mara moja kwa kuwa pia kanuni za utumishi wa umma zinazuia mtumishi kuwa na madeni yaliyopita kiasi.
Aliwataka wataalamu wa Elimu ya Fedha kuwasaidia Watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kuwa na matumizi mazuri ya fedha kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya.
Alisema kuwa elimu ya fedha izingatie kuwasaidia wananchi kunufaika na jitihada zao wanazofanya za uzalishaji na kama ni watumishi wa umma waelimishwe namna bora ya kutumia kipato wanachokipata kupitia mishahara yao, sambamba na wakulima, wafanyabiashara, wavuvi na wengine.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alimhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Timu yake itatoa elimu kwa weledi kwa kuwa miongozo inawataka kuujengea umma uelewa katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini na kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia elimu ya fedha.
Elimu pia inajikita katika kuelimsha wananchi kuhusu umuhimu wa utumiaji wa huduma rasmi za fedha ili kuongeza ujumishwaji wa huduma za fedha, kanuni za kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha, Uwekaji Akiba, masuala ya Mikopo, Hifadho ya Jamii, na kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
Timu ya wataalamu wa Elimu ya Fedha inatoa elimu katika maeneo ya Wilaya zilizopo Mkoa wa Mara ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Bunda, Musoma, Butiama, Rorya, Serengeti na Tarime.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka, akitoa agizo kwa taasisi zenye tabia ya kushikilia kadi za benki za watumishi kama dhamana wanapokopa, kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume cha Sheria, wakati wa mkutano na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, ilipofika ofisini kwake.


Afisa Mipango Wilaya ya Rorya, Sister Sara Mpemba, akieleza mikakati mbalimbali ya kukomesha mikopo umiza kwa kutoa elimu, wakati wa mkutano kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka, na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro (kushoto), katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rorya.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka (kulia) na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa pili kulia), wakitoka katika mkutano ulioangazia namna ya kuwafikia wananchi ili kutoa elimu ya fedha kwa maendeleo yao, uliofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji huyo, Rorya Mkoani Mara.




Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka, akisikiliza maelezo kutoka kwa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa tatu kulia), ilipofika ofisini kwake, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, Bw. Abdul Mtaka (katikati) na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano ulioangazia namna ya kuwafikia wananchi ili kutoa elimu ya fedha kwa maendeleo yao, uliofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi huyo.


Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (kulia) akitoa maelekezo ya eneo zuri la kutolea elimu ya fedha kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo Mkoani Mara.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano. Serikalini, Wizara ya Fedha)