Na Janeth MichuziTv -Dodoma
Wananchi wamepewa wito wa kuchamgamkia kupata nyumba zilizojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambazo zinapatikana kwa bei nafuu, kwa ajili ya kupangisha ili waweze kupata makazi bora na salama.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) Augustine Vuma wakati walipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) zinazojengwa katika eneo la Nzughuni Dodoma.
Vuma, ameeleza kuwa ujenzi wa nyumba 150 kwa awamu ya kwanza umekamilika na ujenzi wa nyumba awamu ya pili ambao unahusisha ujenzi wa nyumba za chini na maghorofa na ukija kukamilika kwa awamu zote utakuwa na nyumba zaidi ya 3000.
Taarifa njema ni kwamba nyumba 150 za ujenzi wa awamu za kwanza zote zimepata wapangaji nani nyumba nzuri na bora sana.
“Nipongeze Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Majengo Tanzania kwa ubunifu huu mzuri mkubwa n awa kimkakati hasa ukizingatia kwamba Dodoma ina wingi mkubwa wa watu hivyo kuwa na mahitaji makubwa sana ya makazi,” amesema
“Mradi unasimamiwa vizuri na tija yake inapatikana tuna matumaini kwamba Wakala wa Majengo Tanzania wataendelea kusimamia mradi huu mpaka utakapokamilika ili kuona ndoto za Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuona watumishi wengi wanahamishiwa hapa wanapata makazi ili waweze kutumika taifa lao kwa ari kubwa.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Mwanahamisi Kitogo aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi amesema, wamepokea maelekezo na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Uwekezaji wa Umma (PIC) na wataenda kusimamia na kutekeleza maelekezo ya kamati.
“Tunaamini mikakati tutayopanga itasaidia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kufanya vizuri zaidi katika usimamizi wa mradi na kuhakikisha maono na mikakati iliyowekwa na serikali inafanyika,” amesema.