Wanandugu wawili wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na shtaka moja la kumuua kwa kukusudia Regina Chaula na kumtupa kwenye shimo la maji taka ndani ya nyumba yake.
Ndugu hao ni Mkulima Mkazi wa Bagamoyo Fred Chaula (56) na Dereva Bodaboda Mkazi wa Tegeta Bashiri Chaula (39)
Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo Leo Machi 13,2025 na kusomewa shtaka lao na Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi kesi hiyo ilipofikishwa kwa mara ya kwanza.
Kabla ya kuwasomea mashtaka yao Mafuru alidai mbele ya Mahakama kuwa washtakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu shtaka wanaloshtakiwa nalo ni la mauaji na Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Washtakiwa kwa pamoja wanashtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu Cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Amedai Februari 18,2025 washtakiwa wakiwa eneo la Bahari Beach ndani ya Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam walimuua kwa makusudi Regina Chaula.
Kwa mijibu wa upande wa mashtaka upelelezi na uchunguzi katika kesi hiyo bado unaendelea hivyo wameomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mushi aliwambia washtakiwa “kama alivyosema awali Wakili wa Serikali kuwa hamtakiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi yenu hivyo na ahirisha kesi hii hadi Machi 27,2025 na washtakiwa warudishwe rumande kwa sababu mashtaka yao hayana dhamana”.
Awali,Fred na Bashiri walikamatwa na Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma za kumuua dada yao Regina wakati akiwa kwenye harakati za kufuatilia kesi zake za madai zilizopo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Dar es Salaam.
Katika taarifa ya Jeshi hilo, ilidai kuwa Januari 18, 2025 askari walifika nyumbani kwa mama huyo na kubomoa shimo la maji take na kukuta mwili wa Regina, baada ya kutilia shaka shimo hilo ambalo lilikuwa limejengewa.