Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amezindua ugawaji wa vitendea kazi,pikipiki 152 na vishikwambi 152 kwa ugani ambao wameajiriwa na bodi ya Korosho kupitia programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT) ili kuwafikia wakulima wa zao hilo kwa urahisi Mkoani Lindi.
Hayo ni katika kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko chanya katika tasnia ya korosho na kuwafanya maafisa hao wanakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa kila mkulima wa korosho na hivyo kuchangia katika kulifikia lengo la uzalishaji wa tani Milion 1 ifikapo 2030 na Tani laki 7 kwa msimu wa korosho ujao.
Akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi huo uliofanyika Machi 13,2025 ,Telack amewahimiza kwenda kushirikiana na wakulima kuondosha changamoto kwenye zao hilo kwa kuhakikisha wanatumia vizuri maarifa waliyonayo kushauri na kutoa mbinu mbalimbali zitakazowawezesha wakulima kulima kwa tija si tu kwa zao la korosho bali hata kwa mazao mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Ndug.Francis Alfred ameeleza kwamba serikali imeamua kuajiri vijana 500 kwa Mikoa ya Lindi,Mtwara,Ruvuma,Tanga na Pwani ambapo kati ya hao Mkoa wa Lindi wamepatiwa maafisa 152 wakiwa na jukumu la kwenda kusimamia shughuli zote za zao la korosho katika vijiji na kata zinazolima zao hilo na mazao mengine.
Pia ameeleza lengo ni kusogeza huduma za ugani kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka Tani 528,262.23 msimu wa 2024/25 hadi kufikia tani 700,000 msimu wa 2025/26 na tani 1,000,000 ifikapo 2030 ikiwa ni jitihada za kuongeza mchango wa zao la korosho kufikia agenda 10/30.
Awali,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Korosho Tanzania Brg Gen Aloyce Mwanjile amesema chimbuko la hayo yote ni maelekezo ambayo yametolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mazao ya kimkakati na kufanyiwa kazi kwa usimamizi mzuri wa Waziri wa Kilimo Husein Bashe ili kuyaimarisha mazao hayo ikiwemo korosho hivyo amewaomba viongozi wote wa ngazi mbalimbali Mkoani Lindi kushiriki kuwasimamia vijana hao ili kupata matokeo chanya.
Baadhi ya maafisa Kilimo ambao wamepatiwa vitendea kazi hivyo licha ya kuishukuru serikali kupitia bodi ya korosho kwa kuwaajiri kwa kipindi cha mwaka mmoja wameomba pia kupewa ushirikiano kutoka kwa maafisa kilimo wa kata husika walizopangwa waweze kutimiza majukumu yao kwa wakulima.