Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa misitu na uhifadhi wa mazingira, wataalamu 10 kutoka Chuo Kikuu cha St. Petersburg nchini Urusi wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano ya kisayansi, kielimu na kiteknolojia kati ya Tanzania na Urusi katika sekta ya misitu.
Akizungumza na Michuzi Blog Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii kutoka SUA, Prof. Agnes Sirima, amesema kuwa ziara hiyo inalenga kutathmini maeneo ya ushirikiano katika sekta ya misitu, hususan kwenye utafiti, teknolojia za misitu, na uboreshaji wa wataalamu katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Prof. Sirima, mashirikiano haya yatatoa nafasi kwa SUA kubadilishana wataalamu, wanafunzi na walimu, pamoja na kushirikiana katika teknolojia mbalimbali za misitu, uchakataji wa mazao ya misitu, na uongezaji wa thamani ya mbao.
“Kama mnavyofahamu, tuna kiwanda chetu cha samani hapa SUA. Tunategemea ushirikiano huu utasaidia kuboresha ufundishaji wa taaluma yetu ya uchakataji wa mazao ya misitu na kuongeza thamani ya mbao,” amesema Prof. Sirima.
Ameongeza kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu kwa wataalamu, walimu, na wanafunzi kujifunza kutoka kwa wenzao wa Urusi, hasa katika teknolojia za kisasa za upimaji wa misitu, ili kuendeleza sekta hiyo na kutoa wahitimu bora wenye ujuzi wa kisasa.
Wataalamu kutoka Urusi wameeleza mafanikio yao katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafiti wa misitu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya satelaiti na drones katika tathmini ya hali ya misitu kwa ufanisi mkubwa. Pia, wamesisitiza umuhimu wa utafiti wa pamoja katika uzalishaji wa miti bora, entomolojia, na usimamizi wa misitu kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI).
Ushirikiano huu unahusisha taasisi tatu kuu: SUA kupitia Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii; Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI); na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS). Ziara ya wataalamu wa Urusi ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kisayansi kati ya mataifa na inatarajiwa kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya misitu nchini na duniani kote.