Wajumbe wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) – Zanzibar leo, tarehe 13 Machi 2025, wamefanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) @officialtea, inayosimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikazi kati ya taasisi hizo mbili.
Ujumbe wa IPA umeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Mhe. Mmanga M. Mjawiri, akiambatana na wajumbe wengine watano, wakiwemo Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Shaaban Mwinchum Suileman.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Bw. Elirehema Mollel, amesema kuwa TEA iko tayari kushirikiana na IPA katika juhudi za kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Aidha, wajumbe wa IPA wameishukuru TEA kwa kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu chuoni hapo katika miaka ya nyuma, huku wakieleza matumaini yao ya kuendelea kupata ufadhili kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, amepongeza IPA kwa utunzaji mzuri wa mradi wa TEHAMA uliowezeshwa na TEA, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi yenye tija kwa maendeleo ya elimu.
TEA ni taasisi ya Muungano inayotekeleza majukumu yake ya kuimarisha miundombinu ya elimu katika maeneo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.