Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezindua Bodi ya Wadhamini
ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuitaka kutekeleza majukumu
yake kwa kusimamia sheria, sera, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali.
Uzinduzi wa Bodi hiyo umefanyika tarehe 14 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi.
Suzanne Ndomba, Naibu Katibu Mkuu TALGWU, Bw. Wandiba Ngocho, Mwakilishi kutoka
Benki Kuu ya Tanzania na Mwakilishi kutoka Msajili wa Hazina pamoja na
Menejimenti ya NSSF.
Mhe. Ridhiwani ameitaka Bodi hiyo pia kusimamia Mpango Mkakakati wa Mfuko
unaozingatia uboreshaji wa huduma ya wanachama, michango, uwekezaji na kulipa
mafao.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unaendelea
kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii na kuwafikia wananchi
waliojiajiri waweze kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao mbalimbali
yanayotolewa na Mfuko.
Amesema suala la wananchi kujiunga na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya
jamii ni ajenda ya dunia na ya nchi na kuwa lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya
Chama, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe, Rais Dkt. Samia
imelipa umuhimu wa pekee.
“Ninakushukuru Mhe. Waziri kwa namna ambavyo umelishikia
bango jambo hili, umeshirikiana na sisi tangu tuanze kampeni yetu ya “NSSF Staa
wa Mchezo” kuhakikisha waliojisajili wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii kama
ambavyo nchi zilizoendelea zimewasajili wananchi waliojiajiri,” amesema Bw.
Mshomba.
Amesema kwa mujibu wa malengo 17 ya dunia, kila lengo linazungumzia masuala ya
hifadhi ya jamii kwa sababu ili uweze kuondoa umasikini ni hatua ya kwanza
wananchi wa taifa husika wawe ni wanufaika wa hifadhi ya jamii, kwa sababu
kupitia hifadhi ya jamii mwanachama au mwananchi wanakuwa na uhakika wa maisha
na kipato.