Meneja wa Kitengo cha Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka Akizungumza katika Mkutano wa Misa Tanzania na Wadau (MISA-TAN – Wadau Summit 2025)
Meneja wa Kitengo cha Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Meneja wa Kitengo cha Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuzingatia maadili ya uandishi na utangazaji wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Akizungumza katika Mkutano wa Misa Tanzania na Wadau (MISA-TAN – Wadau Summit 2025) uliofanyika jijini Dodoma, Mhandisi Kisaka amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa usawa, haki na uadilifu, hasa wakati wa kuripoti habari za vyama vya siasa.
Amesema vyombo vya habari nchini Tanzania vinatakiwa kuzingatia maadili ya uandishi na utangazaji katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, ambapo usahihi na uadilifu wa taarifa ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia.
“Vyama vyote vya siasa vinapaswa kupatiwa nafasi sawa katika kuripotiwa, bila upendeleo. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na zinazowawezesha kufanya maamuzi ya busara”,amesema Mhandisi Kisaka.
Amesema ni muhimu waandishi wa habari kutenda haki kwa kuripoti kile kilichotokea kama kilivyokuwa, na kuepuka kuongeza “chumvi” au kufanya utani kwenye habari.
Mhandisi Kisaka amewataka waandishi na watangazaji kutoandika wala kutangaza habari ambazo hazina ukweli.
Mhandisi Kisaka ameongeza kuwa waandishi wanapaswa kuzingatia kuripoti sera na ahadi za vyama vya siasa, badala ya kujikita zaidi katika matukio pekee.
“Hii itasaidia kuelimisha umma kuhusu mipango ya vyama na jinsi wanavyokusudia kutatua changamoto zinazowakumba wananchi”,amesema.
Picha : MATUKIO YANAYOENDELEA MKUTANO ‘MISA – WADAU SUMMIT 2025’