*RC Chongolo aanika jinsi bilioni 712.3 zilivyotumika kujenga miradi ya maendeleo
Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Songwe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Stephen Wasira amepokea taarifa ya Mkoa wa Songwe ambayo imesheheni lundo la mabilioni ya fedha ambayo yametumika katika miradi ya maendeleo.
Wasira ambaye ameanza ziara ya kikazi katika mkoa huo leo Machi 14,2024 amepokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka kwa Mkuu wa mkoa huo Daniel Chongolo ambaye ameeleza katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wamepokea Sh.bilioni 712.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani wa miradi ya maendeleo katika Mji wa Vwawa Wilayani Mbozi mkoani Songwe, Chongolo amefafanua katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, wamepokea Sh.bilioni 712.3 kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Fedha hizi zimeenda wapi? Dhamira ya Serikali ni kutatua changamoto za wananchi, hivyo fedha ambazo zimetolewa na Serikali zimekwenda katika miradi mbalimbali na sisi tunaona tumependelewa kwa kupatiwa fedha hizi kutekeleza miradi ya maendeleo.Mkoa huu ni mpya lakini yamefanyika mambo mengi makubwa.”
Chongolo amesema katika elimu ya msingi Mkoa wa Songwe zimejengwa shule mpya 78 lakini kuna shule za zamani na shule shikizi ambapo yamejengwa madarasa 345 mapya.
“Kwakipindi kwa kipindi cha maka minne pia walimu wapya 300 wameajiriwa .Nyjmba za 159 zimejengwa kwa ajili ya walimu wa shule za msingi.Hivyo kiasi cha fedha Sh. Bilioni 28.9 zimetumika katika elimu msingi na lengo ni kutatua changamoto.
“Tunakumbuka wakati tunaanza ujenzi wa shule za sekondari za kata mwaka 2005 tulianza kwa kuchanishana na wananchi lakini hivi sasa fedha za ujenzi wa sekondari zote zinatolewa na Serikali moja kwa moja.”
Chongolo amesema katika kipindi cha miaka minne shule mpya 35 za sekondari zimejengwa na madarasa 627 yamejengwa kwa lengo la kusogeza elimu kwa wnanchi.Pia walimu wapya 117 wameajiriwa na nyumba za walimu wa sekondari 182 wameajiriwa.
Pia amesema Serikali imeamua kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita hivyo Sh.bilioni 54.4 zimetumika kuwezesha elimu bila malipo.
Kuhusu sekta ya afya amesema tayari utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa hospitali katika Mkoa wa Songwe inaendelea na kufafanua katika kwa kipindi cha miaka minne wamepokea fedha Sh.bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
“Wakati ujenzi unaendelea na huduma zinaendelea lakini serikali imeleta fedha kujenga hospitali mpya tatu katika Wilaya ya Songwe, Tunduma na Mbozi.Vituo vya afya 18 na zahanati 50 zimejengwa.Pia kuna magari ya kubeba wagonjwa pamoja na pikipiki kurahisisha usambazaji dawa na vifaa tiba.”
Akizungumza kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara, Chongolo amesema Serikali kuna kazi kubwa imefanyika na kufafanua katika kipindi cha miaka saba iliyopita hata Kwenda Ileje ilikuwa anasa lakini leo barabara inapita vizuri.
“Ujenzi wa barabara wa kwenda Isoko unafanyika na lengo ni kuunganisha Songwe na Mbeya kwa njia ya lami upande wa Kyela.Barabara ya Mloo kwenda Kamsamba nayo imeshatolewa kibali sambamba na barabara inayotoka Mbalizi kwenda Kikwajuni na TANROAD wako wako hatua za mwsho kumpata mkandarasi.
“Baada ya kutangazwa barabara hii Rais alitoa maelekezo ijengwa na mkandarasi zaidi ya mmoja, mkandarasi atakayeanzia Mkwajuni na mwingine Mbalizi ili wakutane kati.Kipande cha Kamsamba na Mloo nayo itajengwa na wakandarasi wawili ili wakutane Katikati.lengo kurahisisha usafiri.”
Kuhusu umeme amesema kuwa katika Mkoa wa Songwe vijiji vyote 100 vina umeme na kazi ya kupeleka kwenye vitongoji kazi inaendelea na tayari Serikali imetenga Sh.bilioni 28 kwa ajili ya kusambaza umeme.
“Haijaishia hapo Songwe tunachangamoto ya umeme, unapanda na kushuka, kituo cha kupoza umeme kipo Mbeya umbali wa kilometa 100. Hivyo Serikali imeamua kujenga kituo cha kupoza umeme na tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika wilaya Momba.
“Hivyo umeme utakaozalishwa utauzwa katika nchi ya Zambia kwani wana changamoto ya uhaba wa umeme. Ujenzi wa kituo ulianza Novemba na utakapokamilika hakutakuwa na changamoto ya umeme.”
Kuhusu maji ,amesema upatikanaji maji utakuwa kwa asilimia 78 mpaka asilimia 80 itakapofika mwezi wa sita mwaka huu kwani kuna miradi mikubwa miwili inayoendelea kutekelezwa.
“Tunao mradi wa maji Tunduma ambao tayari umeshatangazwa utakaogharimu zaidi ya Sh.bilioni 100 , mradi huo unachukua maji mto Momba na utakapokamilika hakutakuwa na changamoto ya maji.Katika kilimo wananchi wa Songwe wanajitahidi sana na kwa upande wa mazo ya chakula wanayo ziada ya kutosha kwani wameongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo.
Kuhusu stendi na soko amesema tayari limeshatengwa eneo la Mbimba kwa ajili ya stendi na soko litakalokuwa na hadhi ya soko na stendi ya mkoa.