Morogoro, Machi 2025 – Kampuni ya Airtel Tanzania imejenga mnara wa mawasiliano wa 4G Kijiji cha Idete, wilayani Kilosa, Morogoro, ambao unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wapatao 7000, hatua ambayo itawafungulia fursa wananchi hao kunufaika kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya ujenzi mnara huo katika Kijiji hicho, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema kuwa ujenzi wa minara hiyo iko sambamba na dhamira ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuona Tanzania ya kidjitali na kuona maeneo yote yanafikishiwa mawasiliano.
“Kama alivyosema Mkuu wa Wilaya, kilimo chao wanachokifanya na shughuli zao za kuchunga wanazozifanya wasisumbuke tena kuhangaika kwenda Kilosa mjini. Basi na wenyewe wakae ndani ya mawasiliano waweze kuwasiliana na wateja wao, wauza pembejeo, na waweze kuwasiliana na ndugu zao. Lakini cha muhimu waweze kuwasiliana kama watanzania wengine,” alisema Waziri Silaa.
Aliongeza “Lengo hili sisi wasaidizi wa Rais lazima tuhakikishe hili linatimia. Tunataka tarehe moja mwezi wa nne mnara huu uwashwe na tunataka tarehe 15 mnara huu uzinduliwe rasmi na mnara huu uzinduliwe rasmi na mawasiliano yapatikane hapa idete.”
Waziri Silaa alisisitiza kuwa mnara huo wa mawasiliano sio tu kwa ajili ya wananchi wa Kijiji cha idete bali ni kwa wananchi milioni 8.5 ndani ya nchi ya Tanzania, akiongeza kuwa kabla ya minara hiyo kujengwa wananchi walikosa mawasiliano, lakini Mheshimiwa Rais alitoa fedha ili wananchi hao waweze kupata mawasiliano.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano kwa Umma wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, alisema kuwa wahandisi wanaojenga mnara huo wameeleza kuwa ujenzi huo unatarajia kukamilika mapema na kuwashwa tarehe moja mwezi Aprili mwaka huu.
“Jambo kubwa ambalo timu yetu ya mauzo imefanya tayari mpaka leo wameshapata mawakala wakubwa watatu ambao ni wakazi wa hapa hapa. Kwa hiyo ni ajira ambayo tumeitoa. Lakini bado pia tumepata mawakala wadogo wadogo ambao wanakuwa wanatoa huduma za Airtel money na Airtel Money branch 10 ambaoi tayari tumeshawasajili na tayari wanangojea mnara ule uwashwe waanze kufanya kazi,” alisema Mmbando.
Mmbando aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zinazotokana na mnara huo ambao unajengwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF)