WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo, ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC) nazo kufanya operesheni ya pamoja kufuatilia malalamiko ya uwepo wa bidhaa ambazo hazina ubora na ambazo zinaharibu biashara.
Waziri Dkt. Jafo alitoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kupokea ripoti ya Kamati ya utendaji kazi ya kutathmini mazingira ya ufanyaji biashara baina ya wazawa na wageni nchini.
“Kwa hiyo kuna operesheni za aina mbili ya Idara ya Kazi na wenzao wa Idara ya Uhamiaji pamoja na FCC na TBS, fanyeni kazi hii, wekeni vijana wenu kazini tuwalide Watanzania,” alisisitiza Waziri Dkt. Jafo.
Alishukuru Kamati hiyo kwa kufanyakazi kubwa sana na taarifa ya kamati hiyo ni miongoni mwa taarifa nzito sana.
“Nashukuru taarifa hii mmeileta na majina ya watu waliokuwa wanaitishia Kamati kama mungekuwa legelege msingeweza kufikia hatua,” alisema Waziri Dkt. Jafo.
Alisema kamati hiyo imeleta mapendekezo kadhaa ya muda mfupi, muda wa kati na ya muda mrefu.
Aidha, alisema taarifa imebainisha kuwa jambo ambalo lilikuwa linalalamikiwa ni la kweli. Alisema taarifa imebainisha idadi ya magodauni ambayo yalitembelewa magodauni hayo wanafanyakazi isivyo sawa sawa.
“Lakini mlitembelea maduka ambayo mlibaini watu wengi wanafanyakazi kazi kinyumbe na taratibu, kwa hiyo nishukuru sana kamati hii kwani hamkusita kuchukua hatua, tumesikia watu 31 waliobainika karibu watu 24 waliondolewa hapa nchini, ongereni, hamkutaka kusubiri,” alisema.
Aidha, alisema kamati ilibaini kuwa biashara nyingine japo zinaonekana ni za wageni, lakini usajili wake umefanywa na Watanzaniana.
Dkt. Jafo alielezea kusikitishwa na baadhi ya Watanzania kutoa vitambulisho vyao kwa wageni ikiweme vya NIDA ili kuwawezesha baadhi ya watu wakafanye biashara kinyume na taratibu.
“Hii ni changamoto kubwa ya kukosa uzalendo kwa nchi yako, inashangaza vijana wa kitanzania unatumika katika maizngira kama hayo kuihujumu nchi yako.
Hii ni ishara mbaya maana yake mtu anaweza kubebeshwa hata dawa za kulevya , unatoa uhai wako, thamani yako kwa ajili ya watu wengine?”
Alisema kwenye taarifa hiyo kuna mambo mengi ya hovyo yamebainiaka na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi.