DAKTARI kutoka Hospitali ya Polisi Kilwa Road, Denis Basyagile, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kifo cha Robert Mushi kilisababishwa na kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha mbalimbali mwilini.
Shahidi huyo aameeleza hayo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi inayowakabili aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, na mwenzake Godlisten Malisa, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni dhidi ya kifo cha Mushi.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swalo, Dkt. Basyagile ameeleza kuwa Aprili 23, 2024, alipokea agizo la kufanyia uchunguzi wa mwili wa marehemu Robert Mushi baada ya ndugu zake kufika hospitalini kwa ajili ya utambuzi.
Akiongozwa na wakili wa serikali Asiath Mzamiru kutoa ushahidi wake, Dkt. Basyagile ameeleza…
“Nilipofika mochwari, nilikuta askari aliyekuwa na amri kutoka mahakamani pamoja na ndugu wa marehemu, John Mushi na Magunda. Ndugu walithibitisha kuwa mwili huo ni wa Robert Mushi kwa kumtambua kwa sura.”
Kwa mujibu wa daktari huyo, uchunguzi wa mwili ulifanyika saa 10 jioni, ambapo alibaini majeraha mengi usoni, mikononi, kifuani, tumboni na miguuni. “Sehemu za kifua na nyonga ya kulia zilikuwa zimebonyea, huku mbavu upande wa kulia zikiwa zimevunjika kuanzia mbavu ya tatu hadi ya tisa,” ameeleza.
Aidha, Dkt. Basyagile amebainisha kuwa ini la marehemu lilipasuka, jambo lililosababisha damu nyingi kumwagika kwenye tumbo, huku nyonga yake ya kulia ikiwa imevunjika katika sehemu ya mfupa wa paja. “Chanzo cha kifo kilikuwa ni kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha haya, ambayo mara nyingi hutokana na ajali za barabarani,” ameeleza.
Baada ya uchunguzi huo, daktari huyo aliandika ripoti rasmi na kuikabidhi kwa askari aliyekuwa akisimamia uchunguzi wa tukio hilo lakini ripoti hiyo haikuwa na jina lake.
Hata hivyo mahakama imepokea ripoti hiyo kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alimtaka shahidi kueleza iwapo aliwahoji askari au ndugu wa marehemu kuhusu kilichosababisha kifo chake. Dkt. Basyagile alijibu kuwa hakufanya hivyo.
Aidha, wakili huyo alihoji kuhusu uwepo wa mgongano wa maslahi, ikizingatiwa kuwa hospitali ya Polisi Kilwa Road iko chini ya Jeshi la Polisi, ambalo ndilo linahusiana na kesi hiyo. Hata hivyo, daktari huyo alieleza kuwa hajui kama kilichopelekea uchunguzi ni tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mwili wa marehemu ulikuwa umekaa hospitalini hapo kwa siku 12 kabla ya kufanyiwa uchunguzi. Hata hivyo, daktari huyo hakueleza ni kwa nini ripoti yake haikuwa na majina ya mashahidi waliokuwepo wakati wa uchunguzi huo.
Kesi hiyo inamkabili aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, na mwenzake Denis Basyagile, wakidaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni. Kesi inaendelea kusikilizwa mahakamani.
Jacob na mwenzake wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kusambaza taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma.
Wanadaiwa, Aprili 22 mwaka huu ndani ya mkoa na jiji la Dar es Salaam, Jacob kwa lengo la kupotosha umma , alisambaza taarifa za uongo lkupitia mfumo wa kompyuta wenye jina la Boniface Jacob @ExmayorUbungo wenye kichwa kilichosomeka ‘wenye leseni ya kuua wameua Tena’.
Taarifa hiyo ilieleza ‘kijana wetu Rajabu Mlanga Mushi maarufu kama Babu G, amekutwa Hospitali ya Kilwa Road akiwa ameuwawa. Imagine tumetoa taarifa Jeshi la polisi la kupotelewa kwa kijana wetu , cha ajabu Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likawa linatusaidia kumtafuta pia’
‘Kila siku jeshi la polisi linasema halijapata taarifa wala fununu zozote za kijana wetu na kwamba tuwe wavumilivu wanapambana kuendelea kumtafuta .Jana machale yakawacheza ndugu wa kijana baada ya msiri mmoja kuwatonya ndugu ‘nendeni hospitali ya polisi Kilwa road mkachungulie vyumba vya kuhifadhia maiti’.
‘Ndugu walivyokwenda huko hospitali ya polisi Kilwa road wakamkuta kijana wao akiwa ameuwawa, wahusika wa hospitali wanadai maiti ililetwa tangu tarehe 10 Aprili mwaka 2024, na na askari wa Jeshi la polisi’.
‘Maiti ina siku 12 katika hospitali ya polisi Kilwa road bila jeshi la polisi kujua ipo hapo?…, polisi aliyepeleka maiti ni wa nchi gani?, walipoombwa kujua ni askari wa kituo gani na majina yao ni yapi ,wahusika wa hospitali hiyo ya polisi wanadai hawajui na wanaomba wasitajwe…’.
‘Wacha wanyonge tukazike maiti zetu, sitamani hata kuona ndugu wakiomba uchunguzi dhidi ya maiti yao kwasababu hata mtoto mdogo anajua hapo Muuaji ni nani’.
‘Pili tunajua ile mbinu ya ‘TAPE’, ile kufunga mtu miguu , kufunga mikono kisha kupigwa tape ya mdomo na puano hadi kifo baada ya ile mbinu ya kupeleka msituni ,porini na kupigwa risasi kujulikana. Dar es Salaam ina mtu mmoja katili sana’.
Jacob anadaiwa kusambaza taarifa ya uongo kupitia mfumo wa komoyuta wenye jina la X , kwa jina la Boniface Jacob @ExMayorUbungo wenye kichwa kisomekacho ‘ Mauaji Arusha’.
‘Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii Omary Msamo ameuwawa na skari wa Jeshi la polisi wilaya ya Karatu Mkoa wa Arusha’.
‘Omary Msamo ameuwawa baada ya kusimamishwa na kushushiwa kipigo kizito kilichopelekea kutoa uhai wake na polisi wa usalama barabarani baada ya kutuhumiwa kuendesha gari akiwa ametumia kilevi’.
‘Kwamba, jeshi la polisi linatumia kila jitihada kuzuia vyombo vya habari kuripoti tukio hili kama nia ya kuficha na kuwanusuru askari wake dhidi ya mkono wa sheria’ .
Mshtakiwa Malisa pekee anadaiwa kuwa kwamba, kwalengo la kupotosha umma , alisambaza taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta , kwenye akaunti ya Instagram ya jina la Malisa_gj.
Taarifa hiyo ilisomeka kwamba ‘Aprili 13 Meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @exmayor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024’.
‘Inadaiwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi maeneo ya Kariakoo na baada ya hapo hakuonekana tena’.
‘Leo wakaambiwa nendeni hospitali ya polisi Kilwa road ndugu yenu amefichwa monchwari pale
wakaenda. Lahaula!, wakamkuta Robert akiwa katika jokofu la baridi, hakuwa Robert tena bali mwili wake ukiwa na majeraha ya kipigo’ .
‘Ni mauaji ya kikatili, Maskiki Robert hajawahi kuwa na ugomvi na mtu , kwanini atendewe haya?’.
Kesi hiyo Inaendelea kesho Machi 18, 2025