Na Mwandishi Wetu
BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imeweka bayana msimamo wa kisheria wa Sheria ya Huduma za Habari kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfanya mtu afanye kazi za kihabari kama hajapitia katika taaluma ya Uandishi wa Habari na kukidhi vigezo.
Msimamo huo umebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili Patrick Kipangula leo Jumatatu tarehe 17 Machi, 2025 jijini Dar es Saalam, wakati akizungumza katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One na kujibu swali la mmoja wa wasikilizaji aliyetaka kujua mamlaka ya Bodi katika kushughulikia walio kinyume cha sheria.
Wakili Kipangula amesema kama Serikali na nchi kwa ujumla imekubali kwamba Uandishi wa Habari ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ni lazima kufuata matakwa ya kisheria.
Amesema kuwa hata kama mtu ana kipaji kikubwa kiasi gani, kama hajasoma taaluma ya uandishi wa habari haruhusiwi kisheria kufanya kazi za kihabari.
“Kifungu cha 19 (1) cha Sheria ya Huduma za Habari, kinasema ‘Mtu hataruhusiwa kufanya kazi ya Uandishi wa Habari, isipokuwa mtu huyo awe amethibitishwa kwa mujibu wa masharti ya Sheria’,” amesema Wakili Kipangula na kuongeza.
“Sisi Bodi, tunawashauri na kuwasisitiza wale wote wanaofanya kazi za kihabari bila kuwa na sifa waende shule, wakimaliza watarudi kuendelea na taaluma yao, uzuri ni kwamba mtu kama ana Shahada ya Udaktari anaruhusiwa kusoma Diploma (Stashahada) tu ya Uandishi wa Habari, na huyu anaweza kuwa mwandishi mzuri wa habari za afya,”.
Amesisitiza kuwa Serikali kupitia Waziri mwenye Dhama na Habari wakati huo, ilishatoa muda wa ziada wa miaka mitano ili wale waliokuwa hawakuwa wamesoma warudi shule wakasome, na ulipoisha aliongeza tena mwaka mmoja.
Akijibu swali kuhusu wajibu wa chombo cha habari katika suala la mtangazaji au mwandishi kufanya kazi za kihabari bila kusomea taaluma, Wakili Kipangula amesema chombo cha Habari kina wajibu wa kuajiri watumishi/waandishi waliotimiza vigezo vya kitaaluma kwa mujibu wa Sheria.