Na Said Mwishehe,Michuzi TV -Mbeya
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema Mkoa wa Mbeya umebeba historia kubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, hivyo vijana wa mkoa huo wanalojukumu la kuilinda.
Wasira amesema hayo leo alipokuwa akipokewa rasmi mkoani humo katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya akitokea mkoani Songwe akiendelea na mikutano ya kuzungumza na wanaCCM pamoja na wananchi.
“Nataka niwaambie hapa Mbeya, Chama chetu ni Chama cha historia, sisi ni muungano wa vyama vilivyoikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla, sisi sio chama cha kawaida.
“Vijana ambao hawaelewi ni kwamba sisi ndio tuliosaidia kuikomboa Afrika. Hapa Mbeya ndipo alipopitia Nelson Mandela, hapa Mbeya ndipo alipopitia Sam Nujoma, na wote walipopita hapa kulikuwa na mzee wetu mwanzilishi wa Chama cha TANU alikuwa anaitwa Mwakangale.
“Na yeye ndiye aliewasindikiza kutoka hapa mmoja baada ya mwengine kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwalimu Julius Nyerere…” amesema.
Amesema viongozi hao waliokuwa katika harakati za ukombozi wa nchi zao hatimaye walifanikiwa kuwaondoa wakoloni na kuwawezesha Waafrika kuwa huru.