Benki ya CRDB imefanikiwa kufungua zaidi ya akaunti 380,000 za CRDB AL Barakah hadi kufikia Desemba 2024, huku ikitoa uwezeshaji wa zaidi ya shilingi bilioni 172 kwa wateja wake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa CRDB, Mussa Kitambi, wakati wa hafla ya futari iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chandamali mjini Songea, tarehe 19 Machi 2025. Kitambi ametumia fursa hiyo kuipongeza jamii kwa kuendelea kuichagua benki ya CRDB kuwa mtoa huduma wao.
Ametoa ahadi kuwa CRDB itaendelea kuwa mbunifu ili kukidhi mahitaji halisi ya soko, na kuhimiza wateja kuendelea kutumia huduma za CRDB AL Barakah Banking.
Amesema Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa futari kwa wateja wake na wadau mbalimbali kila mwaka wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo ameeleza kuwa Ramadhani ni fursa ya kujifunza maadili mema, upendo, na mshikamano.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, akiwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwenye hafla hiyo, amepongeza juhudi za CRDB za kuunganisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uadilifu, umoja, na mshikamano katika jamii.
Kwa upande wake, Shehe wa Mkoa wa Ruvuma, Ramadhani Mwakilima, amepongeza jitihada za CRDB na kuwataka benki hiyo kuendeleza hafla za futari ili kuimarisha mahusiano mazuri kati ya benki na wateja, Pia amewashukuru wateja kwa moyo wao wa kujitolea na kuwataka waendelee kuwa sehemu ya familia ya CRDB.
Hafla hiyo imethibitisha dhamira ya CRDB ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake, huku ikisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano katika jamii, ambapo mbali na futari hiyo Benki ilikabidhi sadaka kwa vituo viwili vyakulelea watoto yatima Wilayani Songea.