Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe na mikoa mingine wanaoshiriki kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya Misitu Duniani kushiriki kwenye mdahalo kuhusu Sekta ya Misitu unaoendelea kwenye viwanja vya Saba Saba Mjini Njombe ili kupata elimu ya uhifadhi kutoka kwa wataalam waliobobea katika sekta hiyo.
Mhe. Chana ametoa kauli hiyo leo Machi 20, 2025 wakati alipokagua maandalizi ya Siku ya Misitu Duniani na hatimaye kuongea na washiriki wa mdahalo unaoendelea kwa siku ya tatu sasa katika viwanja vya Saba Saba Mjini Njombe ikiwa ni miongoni mwa shughuli zinazoendelea.
Mhe. Chana aliambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Dunstan Kitandula na Naibu Katibu Mkuu, Kamishina wa Polisi Benedict Wakulyamba.
“Ndugu zangu nawasihi kupokea heshima hii tuliyopewa na Rais wetu kipenzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutuletea maadhimisho haya ili yafanyike katika mkoa wa Njombe.” amefafanua Mhe. Chana.
Aidha, amewataka wananchi wote nchini kushirikiana na Serikali ili kuhifadhi rasilimali zilizopo ikiwa ni pamoja na misitu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Awali, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi ametembelea maonesho maalum ya siku hiyo katika viwanja vya Saba Saba Mjini Njombe.
Maonesho hayo ambayo yanaonyesha mnyororo wa thamani wa Sekta ya Misitu yalizinduliwa juzi ambapo wadau mbalimbali wameshiriki na kuonyesha huduma na mazao mbalimbali yatokanayo na misitu.
Mgeni rasmi hapo kesho ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kauli mbiu ya kitaifa ya mwaka huu ni ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa raslimali kwa kizazi hiki na kijacho.