MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jumatano tarehe 19.03.2025 imekutana na uongozi wa Tanzania Bloggers Netwark (TBN) katika ofisi za TCRA makao makuu Jijini Dar Es Salaam.
Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, TBN imeiomba TCRA kupunguza gharama za usajili wa blogs kama sio kuziondoa kabisa.
Pia TBN imeiomba TCRA iwe inatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa bloggers ili kuwapa ujuzi na uzoefu wa masuala mbalimbali ya kujenga Taifa.
TCRA wamesema kuwa wameyapokea maombi ya TBN na watayafanyia kazi.
“Tunafurahi kukutana nanyi leo, na kujadiliana haya maana Bloggers mna umuhimu mkubwa sana kwenye maudhui ya ndani.
“Kwa mfano Bloggers ni wazalishaji wakubwa wa taarifa muhimu za ndani ambazo husaidia kutumiwa na tasisi za Akili Mnemba (AI) ambazo daima zinatafuta taarifa muhimu wanazopata mitandaoni.
“Nawaahidi tumepokea maombi yenu, tutayafanyia kazi na majibu tutawapatia”, amesema Maneja wa Huduma za Utangazaji Mhandisi Andrew Kisaka.
TBN ni chama cha bloggers kilichosajiliwa rasmi mwaka 2014, kikiwa na wanachama zaidi ya 300 waliosambaa kila kona ya nchi.