
Mkurugenzi wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kwenye mamlaka wa VETA Dkt.Abdallah Shaban akizungumza kwenye kongamano maalum la Maadhimisho ya Miaka 3O la VETA linaloendelea katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi wakipata maelezo kuhusiana na mifumo ya umeme walipotembelea sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya VETA.
Wanafunzi wakisikiliza mada mbalimbali kwenye katika maadhimisho ya miaka 30 ya VETA
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
MAMLAKA ya Elimu na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) imeahidi kufanya maboresho katika mfumo wake wa elimu ya mafunzo ya Ufundi Stadi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.
Maboresho hayo yanahusisha zana za kufundishia kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa na kuajiri walimu wenye ujuzi wa kuweza kuanda vijana katika nyanja mbalimbali za ujuzi wenye ubunifu wa kukabili soko la ajira
Akizungumza katika kongamano maalum lililofanyika leo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kwenye mamlaka hiyo, Dk. Abdallah Shaban amesema VETA inakabiriwa na changamoto ya mifumo ya zamani.
“VETA inakabiliwa na changamoto ya mifumo ya zamani kama matumizi ya mashine za kuchapa (typewriter), huku dunia ikiwa imehamia kwenye matumizi ya kompyuta,” amesema na kuongeza:.
“VETA itashirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha vifaa vya kisasa vinapatikana, sambamba na walimu wenye uwezo wa kufundisha mafunzo yenye kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.”
Pia, ameeleza kuwa VETA inazingatia mahitaji ya watu wenye uhitaji maalumu, ili kuhakikisha kila mtu anapata nafasi ya kujifunza stadi za ufundi.
Katika maonesho yaliyoambatana na kongamano hilo, wanahabari walishuhudia ubunifu na ustadi wa wanafunzi wa VETA, wakiwemo walemavu waliopata mafunzo mbalimbali na kuweza kujiajiri au kuajiriwa.
Miongoni mwa walemavu hao ni Joseph Joachim Mtei, kijana aliyekosa mikono tangu kuzaliwa, lakini kwa kupitia mafunzo ya VETA, ameweza kuwa msanifu majengo na anatarajia kuhitimu mafunzo yake mwezi Desemba mwaka huu.