Na Mwandishi wetu -Dodoma
Wakazi wa kijiji cha Mnenia kilichopo wilayani Kondoa Mkoani Dodoma,wameokoa sh milioni 25 ya fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Mnenia iliopo Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.
Fedha hizo zimeokolewa,baada ya wakazi wa kijiji hiko,kushiriki ujenzi huo kwa kuongeza nguvu kazi ya wanakijiji wa kijiji hiko walioshiriki kujenga madarasa pamoja na matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea shule hiyo,Mwenyekiti wa kijiji cha Mnenia Hassan Mohamed amesema wanakijiji wameshiriki ujenzi huo ili kuhakikisha wanafunzi wanaepuka adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta elimu.
“Tunawashkuru sana TASAF kwa kutujengea shule ya sekondari ya Mnenia,imetusaidia sana kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea kwenda shule za vijiji jirani kwa ajili ya kutafuta elimu,”alisema Mohamed.
Kutokana na hilo amesema,wakazi wa kijiji hiko,wataendelea kushirikiana na TASAF kwa ajili ya kushiriki miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kijiji hicho na maeneo jirani.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF,Peter Ilomo aliswapongeza wanakijini wa kijiji cha Mnenia kutokana na ushirikiano walioonyesha wakati wa ujenzi wa shule hiyo,huku akiwasisitiza waendelee kutunza mazingira ya shule hiyo.
Ilomo amesema nguvu kazi iliotumika kuongeza nguvu ya ujenzi wa madarasa ya shule hiyo pamoja na matundu ya vyoo,ndio itumike pia kuhakikisha shule hiyo inatunzwa vizuri ili itumike na kizazi kijacho.
“Naomba nyie wenyewe mkawe walinzi wa shule hiyo,ili mradi mwingine wa ujenzi unapokuja unaikuta shule hiyo ikiwa imara pamoja na uwepo wa mazingira mazuri,”alisema Ilomo.
Mbali na hilo aliwataka viongozi wa halmashauri ya Kondoa kuwa mstari wa mbele kuiongoza jamii katunza mazingira ya shule hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na vizazi vingine viweze kuitumia.
Naye Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo,Khadija Omary alisema TASAF imekuwa Mkombozi kwa Mamia ya wanafunzi waliokua hatarini kukosa elimu kwa kuhofia kutembea umbali mrefu kutoka kijiji cha Mnenia,kwenda kijiji jirani.
Khadija amesema takribani miaka mitatu sasa wanafunzi wa kijiji cha Mnenia Wilayani kondoa Mkoani Dodoma wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta elimu,lakini hivi sasa shule ya sekondari iko karibu.
Amesema kupitia Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania Tasaf, elimu imesogea jirani hivyo hivi sasa wanafunzi wanasoma shule ikiwa katika maeneo ya jirani.