Na John Mapepele
Kwa mara ya kwanza katika historia ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani ya mwaka huu hapa nchini yanayofanyika katika viwanja vya Saba Saba Mjini Njombe Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa maonesho maalum ya mnyororo wa thamani wa sekta ya misitu pamoja na Wanyamapori.
Kwa vipindi tofauti wakikagua maandalizi ya siku ya Misitu Duniani kwenye maonesho Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Pindi chana na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi wamefafanua kuwa Serikali imeamua kuwaleta Wanyamapori katika maonesho hayo ili kutoa hamasa kwa wananchi kupenda utalii wa ndani.
” Tanzania imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la misitu takribani asilimia 50 ambalo ni makazi ya Wanyamapori, hivyo tumeamua kuwaleta wanyama wananchi waweze kupenda kutembelea hivyo kuliingizia taifa letu fedha.” Amepongeza Mhe. waziri
Naye Dkt. Abbasi amewaarika wananchi kutembelea maonesho ya Wanyamapori hao na kwamba Serikali imetoa fursa ya wanyama hao kuendelea kuwepo katika viwanja hivyo katika siku za mwisho wa juma hata baada ya kilele hapo kesho ili wananchi wengi wapate fursa ya kuwaona.
Mgeni rasmi hapo kesho ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kauli mbiu ya kitaifa ya mwaka huu ni ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa raslimali kwa kizazi hiki na kijacho.