Zaidi ya kiasi cha Shilingi bilioni 300 zimepokewa na kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Ilala, katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita ya Dokta Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Ilala, Mkoani Dar es salaam, Edward Mpogolo, alipozungumza mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya, Elimu, na Miundombinu ya barabara.
Amesema shukrani za pekee ni kwa Rais wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi chake kutoa fedha nyingi kwa ajili ya madarasa ya ghorofa, hospital ya wilaya Kivule, na kuongeza fedha za miradi ya barabara za Tarura.
Amebainisha kuwa fedha hizo zaidi ya Bilioni 300, zilizotolewa zinaenda kukamilisha hospitali ya wilaya Kivule ambayo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya amehakikisha hadi mwezi july itakuwa imekamilika.
Mpogolo, ameendelea kubainisha katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, upande wa miradi ya tarura ameongeza fedha kutoka bilioni tano kwa mwaka hadi bilioni 20 kwa mwaka ambazo zinajenga barabara mbalimbali.
Miradi mingine aliyotembelea Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ni ujenzi wa barabara ya kiwango cha zege eneo la Majohe zaidi ya mita 400 ambayo pia yapo mapato ya ndani ya jiji kwa asilimia 10.
Ameeleza Barabara ambazo zinajengwa kwa sasa maeneo mbalimbali zinawekwa taa, makaravati na mitaro kwa ajili ya upitishaji maji.
Mpogolo amesisitiza fedha zilizopokewa ni nyingi na zinaonyesha matokeo chanya katika miradi ya maendeleo kwa wananchi wilayani Ilala.
Mradi mwingine kwa wananchi wa Ilala ni Dmdp awamu ya pili ambao ni wa zaidi ya kilometa 11, na tayari mkandarasi amepatikana na kashalipwa malipo yake ya awali ili kuanza kazi ya ujenzi katika kata ya Kitunda, Kivule, hadi Msongola.
Kazi ambayo Mkandarasi anaanza muda wowote kuanzia sasa kwa barabara zilizokuwa na changamoto.
Barabara nyingine inayokwenda kukamilishwa kwa kiwango cha lami ni Mzinga hadi Kitunda ambayo mkandarasi atajenga kilometa moja.
Jambo ambalo Mpogolo ameendelea kumshukuru Rais wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi cha miaka minne halmashauri ya jiji la Ilala, imepokea fedha kiasi cha shilingi bilioni 317 zilizowezesha kujenga zaidi ya madarasa 600 shule za Sekondari na zaidi ya madarasa 400 shule za Msingi.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameeleza kutokana na kazi kubwa aliyofanya Rais wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan kuna kila sababu ya kumpa kura za kutosha katika uchaguzi wa mwezi wa kumi mwaka huu.
Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la Mpiga kura linaloendelea Mkoani Dar es salaam.