*Hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa watu wenye ujuzi na ufundi stadi
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ina uwezo na jukumu la kuibadilisha Tanzania kwa vijana kupata stadi kwa ajili ya kuboresha maisha yao.
Dk. Biteko ameyasema hayo leo Machi 21,2025 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 30 ya VETA yaliyohitimishwa jijini Dar es Salaam.
Amesema ni kawaida kuona mtoto aliyemaliza kidato cha sita au ana digrii ya elimu hawezi kujipikia chakula chake mwenyewe, kufua nguo bali anataka kuhudumiwa hapo hatuwezi kuendelea na kizazi hicho.
Dkt.amesema hakuna nchi yeyote duniani iliyoendelea bila kuwa wataalam wenye ujuzi na ufundi kutokana na watu hao waliweza kuonyesha ujuzi wa kuunda vitu mbalimbali.
“Niliwatania watu fulani kuwa mnazalisha maofisa wa kuhudumiwa badala ya watu wa kuja kuhudumia jamii jambo ambalo ni hatari katika taifa na VETA mnayo nafasi kubwa ya kuziba hili pengo,
“Tunauwezo mkubwa wa kubadilisha nchi yetu kama wote tutakubaliana kwamba watoto wetu wapate stadi fulani kwa ajili ya kubadilisha maisha yao, na katika elimu tuangalie watoto wanapenda nini na kuwaelekeza kwenye hicho wanachopenda, hakuna taifa lolote duniani ninalolifahamu ambalo limeendelea bila kuwa na watu wenye stadi fulani za kuweza kutatua matatizo yao,” amesema Biteko na kuongeza
“Tukiacha kuwekeza kwenye kufundisha watoto wetu stadi maana yake tutatafuta stadi hizo nje ya nchi kwa gharama kubwa na matokeo yake kazi zozote iwe kujenga barabara au nyumba zitakuwa na gharama kubwa kwa sababu ujuzi au ufundi huo haupatikani ndani ya nchi,” amesema
Aidha Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali imeweka msukumo mkubwa katika ufundi stadi ili Watanzania wapate elimu yenye viwango vikubwa na ujuzi wa kuweza kujikomboa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anajenga VETA kila wilaya ili kuwapa ujuzi watanzania waweze kuajirika katika sekta zote,” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Hata hivyo, ameipongeza Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa kuwa na maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa hatua hiyo kubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi ili kuwajengea uwezo watanzania katika ujuzi mbalimbali.
“Kwa mara myingine nawapongeza VETA kwa kuendelea kutoa mafunzo na ujuzi kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuhakikisha kuwa ujuzi unatolewa kwa kuzingatia ubora na viwango vya kimataifa, ” Amesema Dkt. Biteko.
Vile vile, amesisitiza elimu kutolewa kwa watu wenye mahitaji maalumu na wanaotoka kwenye mazingira magumu nchini yaweze kuongeza fursa kwa kila mtanzania kupata elimu ya ujuzi.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kwamba, Maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA ni uhalisia kuwa Serikali imeipa kipaumbele VETA ili vijana wapate elimu ikiwemo kujenga vyuo vya ufundi katika maeneno mengi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA, Anthony Kasore amesema kuwa, VETA imezingatia viwango na ubora wa mafunzo unazingatiwa ili vijana wanaohitimu waweze kumudu soko la ajira.
Aidha amemshukuru Rais Samia kwa usimamizi na uwezeshaji wake mkubwa katika mafunzo ya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata maarifa na ujuzi ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa tija.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akizungumza wakati kufunga Maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA ,jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore akizungumza kuhusiana maadhimisho ya miaka 30 na namna watavyofanyia kazi maoni katika kuboresha utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi stadi jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya VETA ,jijini Dar es Salaam.