*Achangisha zaidi y ash. Milioni
600 katika harambee ya ujenzi wa maktaba, madarasa ya amali na ukumbi kwa ajili
ya Seminari ya Agape
*Asema lengo ni kujenga
jamii madhubuti na yenye kujitambua
*Asisitiza sekta ya elimu
ni wakala wa mabadiliko
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imeweka kipaumbele kikubwa cha uwekezaji katika sekta ya elimu nchini
ili kujenga jamii madhubuti, yenye kujitambua, kujitegemea, kujiheshimu na
kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu.
Ameyasema hayo jana (Alhamisi, Machi 20,
2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika harambee
ya ujenzi wa maktaba ya kisasa, ukumbi wa mikutano na madarasa ya amali ya
shule ya Seminari ya Agape inayomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya
Kaskazini.
Katika harambee hiyo iliyofanyika kwenye
Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam ambapo zaidi ya shilingi milioni 600
zilikusanywa ikiwa ni ahadi na fedha taslimu, Waziri Mkuu alisema sekta ya
elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni
katika kuleta maendeleo ya nchi.
“Harambee hii ni hatua muhimu katika
kuhakikisha kwamba tunafanya uwekezaji mkubwa katika elimu ya watoto wetu.
Maktaba na madarasa ya amali katika Sekondari ya Agape yataleta manufaa mengi
yenye tija kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.”
Alisema ni muhimu kutambua kwamba bila ya
uwekezaji mzuri katika elimu, hatuwezi kufika mbali. “Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuunga
mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazochangia katika ujenzi wa Taifa letu.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuwa na
vijana wenye maarifa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kijamii, kitaifa
na kimataifa inahitaji kuwa na sekta ya elimu iliyo bora, imara na inayokidhi
mahitaji ya jamii.
Waziri Mkuu amesema ili kuongeza fursa za
elimu kwa Watanzania wote, Serikali imeongeza idadi ya shule za msingi kutoka
16,656 mwaka 2020 hadi 19,783 mwaka 2024 na shule za sekondari kutoka 5,001
mwaka 2020 hadi 5,926 mwaka 2024.
Naye,
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amelipongeza KKKT kwa
kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Awali,
Mhashamu Baba Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Fredrick Shoo alitumia
fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya maboresho ya sekta ya elimu
nchini. “Ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia kwa maboresho ya sera ya elumu
pamoja na ujenzi wa shule na ufadhili wa masomo ya sayansi.”
Akizungumzia kuhusu harambee hiyo alisema
inalenga kukusanya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi maktaba ya kisasa,
madarasa ya amali pamoja na ukumbi anuwai katika shule ya Seminari ya Agape ili
kuunga mkono maboresho yaliyofanyika katika sera ya elimu.