CHAMA cha Walimu Tanzania(CWT) Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,kimeipongeza Serikali ya awamu ya sita,kwa kuruhusu walimu kupandishwa madaraja kwa wakati,kupata daraja la mseleleko na kulipa viwango vipya vya mishahara.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Katibu wa Chama hicho Neema Lwila,wakati akisoma risala ya Walimu kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Manispaa ya Songea uliofanyika katika ukumbi wa Anglikana mjini Songea.
Lwila alisema,awali walimu waliokuwa na ajira ya pamoja na hawakuwa na mashauri ya kinidhamu waliachana kimadaraja,lakini sasa tatizo hilo limetatuliwa na linaendelea kutatuliwa baada ya Serikali kukaa na kujadiliana na Chama cha Walimu kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga shule mpya zaidi ya 600 za Msingi na Sekondari,kuboresha miundombinu hususani ukarabati wa madarasa na nyumba za walimu,kuajiri walimu wapya na kuanza kulipa madeni ya walimu.
Lwila,ameipongeza Serikali kuanza kulipa madeni hayo, hata hivyo alieleza kuwa bado walimu wanadai fedha nyingi na ameishauri Serikali kuwabana Wakurugenzi wa Halmashauri kutumia mapato ya ndani kulipa madeni ambayo siyo ya mishahara.
Akizungumzia upungufu wa walimu Lwila alisema,Manispaa ya Songea ina idadi ndogo ya walimu na baadhi ya shule zina walimu wasiozidi watano ambao hawakidhi mahitaji.
Alisema,walimu hao wakiingia kwenye kipindi kimoja baadhi ya madarasa yanabaki bila walimu hali inayopelekea ufaulu mbovu hasa kwa elimu ya awali na msingi.
Kwa upande wake Afisa elimu msingi Manispaa ya Songea Hossen Mghema,amewataka walimu kutanguliza uzalendo kwa Chama na kuiunga mkono Serikali iliyopo madarakani ambayo katika kipindi cha miaka minne imefanya maboresho mbalimbali mazuri kwa walimu.
Kwa mujibu wa Hossen,baadhi ya maboresho yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa walimu ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia,ujenzi wa nyumba za walimu na kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Hata hivyo,amewaomba walimu na wanafunzi,kutunza miundombinu inayojengwa kwenye shule zao ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwani Serikali inatumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwenye ujenzi wa miradi mingine a maendeleo.
Akizungumzia kuhusu upandashaji wa madaraja Hossen alisema,Serikali kupitia Halamshauri ya Manispaa ya Songea inaendelea kupandisha madaraja kwa walimu na watumishi wa kada nyingine kulingana na sifa zao sambamba na kulipa madeni.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Manispaa ya Songea ambaye alichagulia katika kipindi kingine cha miaka mitano Emmanuel Komba,amewataka walimu kuwa waadilifu,kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuongeza kiwango cha taaluma na kuepuka migogoro isiyokuwa na tija sehemu ya kazi.
Amewashukuru walimu kwa kumuamini na kumchagua tena kushika nafasi hiyo na kuhaidi kutoa ushirikiano mkubwa kwao katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya elimu ili kwa pamoja waweze kufanikiwa hasa kwenye maslahi yao.