Zanzibar, 22 Machi, 2025– Benki ya Equity siku ya jana iliandaa tukio la kipekee la Iftar, likiwa na lengo la kuleta pamoja wadau muhimu, wakiwemo viongozi, wateja, na wadau mbalimbali, ili kusherehekea kwa pamoja katika mwezi huu wa Ramadhani. Iftar hiyo ilifanyika katika hotel ya Madinat Al Bahr.
Katika hotuba yake, Bw. Haidari Chamshama, kwa niaba ya Menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya Equity, alikaribisha wageni na kutoa shukrani za dhati kwa wote waliohudhuria tukio hili. Shukrani za kipekee zilielekezwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mh.Omary S. Shaaban, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo.
“Ni furaha kubwa kuwa na wewe hapa leo, Mheshimiwa Waziri,” alisema Bw. Haidari Chamshama, Mkuu wa Kitengo cha Malipo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Equity Tanzania. “Uongozi wako umejikita katika kukuza sekta ya biashara na viwanda Zanzibar. Juhudi zako ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wetu, na sisi kama benki tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii ya maendeleo.”
Tukio hili lilikuwa fursa ya kuonyesha shukrani kwa wateja waaminifu wa Benki ya Equity, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya benki. “Kama benki, tunatambua kwamba hatuwezi kufanikiwa bila ya ushirikiano wenu. Leo hii, tunasherehekea mafanikio yetu kwa kushirikiana nanyi, na tunaendelea kujitahidi kuboresha huduma zetu kila siku,” aliongeza Bw. Haidari Chamshama, Mkuu wa Kitengo cha Malipo aliyeongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Equity Tanzania.
Katika kipindi cha Ramadhani, ambapo mshikamano, kusaidiana, na huruma kwa wengine ni muhimu, Benki ya Equity imejizatiti kutoa huduma bora kwa jamii. Benki inatambua na inajivunia katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma zetu bora na bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja wake. Na tunaahidi kuendelea kuleta huduma bora zinazoendana na kasi ya tekinolojia.
Kwa kumalizia, Bw. Haidari Chamshama aliwaomba wadau na wateja wote waendelee kutumia huduma za benki na kuwatakia Ramadhan njema. “Kwa niaba ya Benki ya Equity, natakieni Ramadhani yenye amani, furaha, na mafanikio. Mfungo wenu uwe wa baraka na mafanikio.”
Tukio lilimalizika kwa dua na Iftar, ambapo wageni walifurahia mshikamano na roho ya kujitolea.