Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar.
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuzindua ripoti maalum inayoangazia nafasi za wanawake katika uongozi wa michezo.
Ripoti hiyo, iliyozinduliwa katika ofisi za TAMWA Z huko Tunguu, Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), imebeba kauli mbiu “Ushiriki wa wanawake na wasichana ni kichocheo cha maendeleo.”
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Bodi ya TAMWA Z, Asha Abdi, anaeleza kuwa tatizo la ukosefu wa uongozi wa wanawake lipo si tu katika michezo, bali katika sekta nyingi.
“Wanawake bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kufikia nafasi za uongozi katika kila sekta. Hali hii inahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia unafikiwa”.
Afisa Programu wa TAMWA Z, Khairat Haji, anasema utafiti umebaini kuwa wanawake bado wako nyuma katika nafasi za uongozi kwenye sekta ya michezo.
“Ripoti imeonesha jinsi wanawake walivyo nyuma katika nafasi za uongozi kwenye michezo, hali inayotokana na changamoto mbalimbali, zikiwemo unyanyapaa, ukosefu wa fursa, na mfumo dume unaotawala sekta hii,” anasema Khairat Haji.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Afisa Ufuatiliaji wa TAMWA Z, Mohammed Khatib, alieleza kuwa tafiti zinaonesha changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake katika sekta ya michezo, ikiwemo manyanyaso na unyanyapaa.
“Ripoti imebaini kuwa kati ya wanawake 102 waliohojiwa, asilimia 12 wamepitia udhalilishaji kutoka kwa makocha, asilimia 16 wamekumbwa na matusi na kashfa, na asilimia 12 wanategwa wanapokuwa kwenye hedhi,” anawasilisha Mohammed Khatib.
Akichangia mjadala huo, Ukht Amina Khalfan kutoka Kitengo cha Michezo na Utamaduni, alikanusha dhana kuwa dini inazuia ushiriki wa wanawake katika michezo na uongozi.
“Dini haijakataza michezo wala haijazuia wanawake kushiriki katika uongozi wa michezo. Tunahitaji kuelimisha jamii kuhusu nafasi ya wanawake katika michezo bila kuhofia vikwazo vya kijamii,” anasema Amina Khalfan.
Kwa kuhitimisha hafla hiyo, TAMWA Z ilisisitiza kuwa ripoti hii inapaswa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya michezo Zanzibar, kwa kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa sawa na kushiriki kikamilifu katika uongozi wa michezo.
Kwa upande wake, Afisa Michezo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Khatima Mwalim, anasema kuwa moja ya changamoto kubwa inayoathiri maendeleo ya wanawake katika michezo ni mtazamo hasi wa jamii.
“Dhana ya kwamba michezo ni uhuni ndiyo inayorudisha nyuma wasichana wengi kuendelea mbele katika sekta hii. Tunapaswa kubadilisha mtazamo huu ili kutoa fursa sawa kwa wote,” Khatima aliweka msisitizo.
Naye Talib Ramadhani, mhamasishaji wa masuala ya wanawake na uongozi, anasisitiza kuwa wanawake wanapaswa kupewa nafasi za kuanzisha na kuendeleza ligi za michezo ili kuleta mabadiliko katika sekta hiyo.
“Wanawake wamekuwa nyuma hata katika kuanzisha ligi na kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya michezo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa wanapewa nafasi ya kushiriki na kuongoza pia”.
Ripoti hiyo pia imeonesha idadi ya wanawake waliopo katika vyombo mbalimbali vya uongozi kwenye taasis zinazojishughulisha na michezo Zanzibar. Katika Baraza la Michezo Zanzibar lenye nafasi 15, wanawake ni wanne. Kwa upande wa ZFF, kati ya nafasi 16, mwanamke ni mmoja na msichana mmoja pekee. Hata hivyo, katika Chama cha Netball Zanzibar, wanawake ni nane huku wanaume wakiwa watano, hali inayoonesha kuwa bado kuna mwamko mdogo wa wanawake kushiriki kwenye uongozi wa michezo.