Na Belinda Joseph, Songea Ruvuma.
Wakazi elfu 5883 wa maeneo ya Sinai na Londoni Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji , wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia 14 Februari 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026 wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Mhandisi Jafari Yahaya, wakati akitoa taarifa za mradi huo kwa wananchi wa Mtaa wa Londoni na Sinai Manispaa ya Songea kwa nyakati tofauti tofauti, katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya maji, amesema kuwa mradi huo umekwisha sainiwa tangu tarehe 13 Januari 2025 kati ya SOUWASA na Mkandarasi Estate Constructor Co. Ltd na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Ameeleza lengo la mradi huo ni kuboresha miundombinu ya majibkwa kusambaza mabomba mapya ya maji safi, kuongeza kiwango cha maji kinachotolewa kwa wananchi kwa ufanisi na uhakika, pamoja na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kupunguza umbali wa kutafuta maji.
Kadharika faida za mradi huo ni kuimarisha huduma za maji kwa wakazi wa Sinai na Londoni, kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama, kuboresha hali ya usafi wa mazingira na maisha ya wananchi kwa ujumla na kupunguza muda unaotumika kutafuta maji hasa kwa wanawake na watoto.
Akizungumza Diwani wa Kata ya Lilambo Yobo Mapunda, amesema wamekuwa wakijadiliana kwa muda mrefu na Mamlaka hiyo kwaajili yakufikisha maji kwa wananchi wa Sinai na Mang’ua lakini kwasasa Anafurahi kuona tayari mafundi wamekwishaanza utekelezaji na rai yake kwa SOUWASA nikuhakikisha wanasimamia ipasavyo mradi huo mpaka kukamilika kwake ili kuwawezesha wananchi kuanza kutumia huduma hiyo
Mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na serikali na jamii ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa wote na unagharamiwa na serikali ya Tanzania kupitia bajeti ya maendeleo ya sekta ya Maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025.