Ndola, Zambia:
Mwenyekiti wa Bodi ya ya Wakurugenzi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya leo
23 Machi 2025, ameongoza wajumbe wa Bodi hiyo na Menejimenti kwenye
ziara ya kutembelea Bomba la Mafuta la TAZAMA linaloanzia Dar es Salaam,
Tanzania hadi Ndola, Zambia. Ziara hiyo ilianza Machi 21, 2025.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Nishati ya Bodi hiyo, Mha. Ngosi Mwihava alisema lengo la
ziara hiyo ni kutizama utekelezaji wa masuala ya kiuchumi, kimiundombinu
na uendeshaji wa bomba la TAZAMA.
“Moja ya jukumu la EWURA
katika sekta ya petroli ni kudhibiti miundombinu ya usafirishaji wa
mafuta na gesi asilia, hivyo ziara hii ni mahsusi kwa ajili ya
kutembelea miundombinu ya bomba, kuona changamoto zilizopo na kuangalia
namna tunavyoweza kusaidia utatuzi wa changamoto hizo ili kuendelea
kuboresha huduma za usafirishaji wa mafuta kupitia bomba hili” alisema.
Mha.
Mwihava aliongeza kuwa, ziara hiyo ni fursa kwa Bodi ya EWURA na ya
Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) kubadilishana uzoefu katika maeneo
mbalimbali ikiwemo ya upangaji wa bei, mikakati ya uhifadhi wa mafuta ya
akiba na kujengea wataalamu uwezo.
Ujumbe huo pia, umetembelea
kituo cha Chilolwa cha kuangalia usalama wa bomba la mafuta, kituo cha
kusukuma mafuta kilichopo Chinsali na ghala la kuhifadhia mafuta
lililopo Mpika.
Maeneo mengine yaliyotembelewa ni kituo cha
Kilonje cha kusukuma mafuta, kituo cha Mulilima cha kutuma na kupokelea
kifaa cha kufanya usafi wa bomba, na kituo cha kupokelea mafuta cha
Bwana Mkubwa ambacho kiko Ndola.
Ujumbe huo pia utakutana na
uongozi la Bomba la TAZAMA, Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Udhibiti
wa Nishati Zambia (ERB) pamoja na Baraza la Udhibiti wa Huduma za Maji
na Usafi wa Mazingira Zambia (NWASCO) ili kujadili masuala mbalimbali ya
ushirikiano wa kisekta.