Na Muhidin Amri,Songea
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile,ametoa Ushauri kwa Msajili wa Vyama
vya Wafanyakazi Nchini, kutafakari upya kuhusu kuwepo kwa Chama zaidi
ya kimoja cha wafanyakazi wa kada moja ili kuondoa migogoro na migongano
inayochangia kushuka kwa nidhamu sehemu ya kazi.
Ndile amesema hayo jana,wakati akizungumza na walimu kwenye Mkutano wa
mwaka wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Halmashauri ya Wilaya Songea
uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Anglikana mjini Songea.
Alisema,uwepo wa chama zaidi ya kimoja kinachohudumia walimu wale wale
ambao ni watumishi wa Serikali inapelekea kuwa na mashindano kati ya
kiongozi wa Chama kimoja na kingine hivyo kutoheshimiana na kushusha
morali ya kazi kwa walimu.
“ Kwa mfano unakwenda shule ya Sekondari Maposeni au Mfaranyaki
unakutana na viongozi wawili wa chama cha wafanyakazi,mmoja anatoka
Chama cha Walimu Tanzania na mwingine wa Chama iko kingine,hii inaleta
madhara makubwa katika utendaji kazi kwenye sekta ya elimu”alisema
Ndile.
Alisema,viongozi hao hawafanyi kazi ya kutetea maslahi ya walimu bali
watafanyakazi kwa kushindani ili kupata wafuasi wengi zaidi,jambo
ambalo ni kinyume na falsafa ya Chama cha wafanyakazi.
Alisema,msingi wa kuundwa kwa Chama cha Wafanyakazi ni kuunganisha
nguvu zao ili wawe na sauti moja, lakini walimu kwa kupitia Chama chao
wanakwenda kinyume hali iliyosababisha hata nidhamu kushuka kutokana na
kugawanyika makundi mawili.
“Heshima ya walimu kwa sasa imeshuka kutokana na kuwepo kwa chama
zaidi ya kimoja kinachotetea walimu hatua inayopelekea baadhi ya walimu
kutoheshimiana sehemu ya kazi.”alisema Dc Ndile.
Amewataka Walimu kuungana na kuwa kitu kimoja na kutetea maslahi
yao,kudumisha nidhamu na kuheshimu mamlaka za utezi ili kujenga kizazi
chenye maadili mema na viongozi bora.
“Lazima mamlaka tuziheshimu, tuache tabia ya kutunishiana misuli,watu
wa namna hii hasa Viongozi wanawaharibia nyinyi walimu, Serikali
inawapenda sana ndiyo maana inaendelea kuboresha maslahi yenu ikiwemo
suala la mishahara,mazingira bora ya kufundishia na kutoa vifaa vya
kufundishia”alisema Ndile.
Awali Katibu wa Chama cha walimu Halmashauri ya Wilaya Songea Adriano
Ngairo alisema, walimu zaidi ya 255 wamefukuzwa uanachama baada ya
kwenda kinyume na maadili ya chama hicho.
Aidha alisema,katika kipindi cha miaka minne jumla ya walimu 440
wamepanda madaraja ya mseleleko,kuruhusu walimu kupandishwa madaraja kwa
wakati kutokana na mwongozo na ameishukuru Serikali kwa maboresho hayo
yaliyowezesha kurudisha moroli ya kazi kwa walimu.
Ngairo,ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu hususani
ukarabati wa madarasa,nyumb za walimu na ujenzi wa shule mpya zaidi ya
600 hapa nchini na kutoa fedha za uendeshaji wa taasisi(Captation) kwa
shule zote nchini.
Ameiomba Serikali kupitia taasisi ya kuzuia na kupambana na
rushwa(TAKUKURU)na idara nyingine za Serikali kushiriki kwa pamoja
kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa miundombinu ya
shule ili kuepuka migongano inayopelekea baadhi ya walimu kukamatwa kwa
kuonekana kushindwa kusimamia miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama
Ndilea,kifungua Mkutano wa Chama cha Walimu wa Halmashauri ya Wilaya
Songea katika Ukumbi wa Anglikana Songea mjini.
Mjumbe wa
kamati ya utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania anayewakilisha
Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila,akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama
cha Walimu Halmashauri ya Wilaya Songea.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania Mkoa wa
Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile wa pili
kushoto baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho katika Ukumbi wa
Anglikana Songea Mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile katikati,akiwa
katika Picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania wa Mkoa
wa Ruvuma na Wilaya ya Songea baada ya kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa
Chama hicho jana.