NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Kuna mafanikio makubwa katika Sekta ya Maji nchini, upatikanaji wa maji vijijini hadi sasa ni asilimia 83 ikiwa imebaki asilimia 2 tu kutimiza ahadi iliyotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025. Vile vile upatikanaji wa maji mjini ni asilimia 95.
Ameyasema hayo leo Machi 22, 2025 Jijini Dar es Salaam Rais Dkt. Samia Hassan katika Kilele cha Wiki ya Maji na Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2022 Toleo la Mwaka 2025 ambapo wadau mbalimbali wameweza kushiriki.
Amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyoshuhudiwa nchini, ni lazima baadhi ya masuala yabadilike ili wananchi waendelee kunufaika na upatikanaji endelevu wa maji safi na salama.
Aidha amesema kuwa katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maji iliyoboreshwa, Serikali inapaswa kujihadhari dhidi ya matishio kwa usalama wa chakula, athari za mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya siasa za dunia.
Ili kuwa na upatikanaji wa maji endelevu lazima wananchi washirikiane na Serikali kutunza na kulinda vyanzo vyote vya maji ikiwemo miundombinu ya maji iliyojengwa kwa gharama kubwa na ili kuepusha madhara kwa afya ya watumiaji wa maji ikiwa mabomba yatapasuka.
Kila tone la maji lina thamani, iwe maji ya mvua au ya mto. Tutumie utaalamu uliopo kuvuna maji hayo, kwa sasa mambo ni rahisi, nimeona vijana wana teknolojia nyingi za uvunaji wa maji ya mvua tofauti na miaka ya nyuma, tuzitumie.
Pamoja na hayo amemuagiza Waziri wa Maji kuanzisha Gridi ya Maji ya Taifa kama ilivyo Gridi ya Taifa ya Umeme, lengo ni kuwa na vituo vya kupokea maji kutoka vyanzo mbalimbali vya maji nchi nzima kwa kuwepo vituo vya Kanda kisha kuwepo utaratibu wa kusambaza maji nchi nzima.


