Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania imemtangaza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili Prof. Mohamed Yakub Janabi kuwa Mgombea wa Nafasi ya
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Akibainisha
sifa na uwezo binafsi wa mgombea huyo katika mkutano na waandishi wa
habari, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb.) amesema kuwa Prof.
Janab ni mgombea sahihi mwenye uwezo wa kazi na kufanya mageuzi pamoja
na maboresho katika sekta ya afya.
Aidha, ameeleza kuwa Prof.
Janabi amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwa ni pamoja
na kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo
ameshiriki katika kuleta mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma bora za
afya na kuimarisha mifumo ya rufaa kutoka vituo vya kutolea huduma za
afya ngazi ya msingi mpaka Taifa.
Vilevile amesema kuwa, akiwa
Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza na mwanzilishi wa Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Janabi aliongoza mageuzi makubwa katika
huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania na barani Afrika. Mageuzi
haya yameleta mafanikio makubwa, ikiwemo kupungua kwa asilimia 95 ya
rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, na kuimarisha utoaji wa
huduma za matibabu ya moyo katika kanda ya Afrika.
“Tanzania,
kupitia mgombea wetu, Prof. Janabi, ina imani kubwa ya kushinda katika
uchaguzi huu kutokana na maono yake ya kuunganisha nguvu za pamoja kwa
ajili ya kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya barani Afrika.
Uzoefu wake wa muda mrefu katika sekta ya afya, uongozi wake madhubuti,
na mchango wake mkubwa katika maboresho ya huduma za matibabu ndani na
nje ya nchi, ni vigezo vinavyomfanya kuwa kiongozi bora wa kuboresha
afya ya wananchi wa Afrika,” alifafanua Waziri Mhagama.
Waziri
Mhagama pia, ametoa wito kwa Watanzania na wadau wa sekta ya afya
kushirikiana katika kumnadi Prof. Janabi, akisisitiza kuwa ushindi wake
utasaidia kuimarisha mifumo ya afya Afrika na kuhakikisha upatikanaji wa
huduma bora kwa wananchi wote wa bara hili.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb.) akimnadi mgombea Prof. Janabi nafasi ya Mkurugenzi wa Who Kanda ya Afrika.