Na Mwandishi wetu -Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Peter Ilomo ametembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya Wangi -Wotta Halimashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma ambapo lengo la kutembelea mradi huo ni kuona ujenzi huo ulipofikia na kuzungumza na Wananchi wa eneo hilo pamoja na wanufaika wa TASAF.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Taifa ya Uongozi (TASAF) amesema ni jambo jema kuona fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi zimetumika vizuri na nimatumaini yake Kuwa kituo hicho cha afya kitatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa,
“Nafaham changamoto mlizopata katika utekelezaji wa mradi niwaombe tuendelee kusimamia vizuri mradi ukamilike kwa ajili yetu sisi tuliokuwepo leo na kizazi kijacho,” alifafanua.
Ilomo amesema zipo kazi ambazo zitafanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa na Wizara ya Afya ina miongozo yake kwa ajili ya vifaa vinavyotakiwa vifike katika kituo hicho
“Kwa muda mfupi tulionao kufikia mwezi septemba wakati wa kufunga mradi tufanye kazi usiku na mchana ili mradi uweze kukamilika ili kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri tuweze kutoa huduma,” alibainisha.
Awali afisa Mtendaji wa kijiji Amoni Mdajile amesema Jitihada za serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ulianzisha ujenzi wa kituo cha afya Wangi ulijumuisha majengo nane, jengo la maabara, jengo la mama na afya ya mtoto, jengo la kufulia, jengo la watumishi wa afya, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la kuchomea taka.
Mdajile amesema mradi wa Ujenzi kituo cha afya ulitakiwa kukamilika mwezi wa pili 2025 lakini kutokana na changamoto za upatikanaji wa vifaa vya ujenzi sasa unatarajiwa kukamilika mwezi wa nne mwishoni 2025.
“Walengwa wamenufaika kwa namna mbalimbali na fedha za ruzuku kulingana na mpango huu kwa kuongeza ujuzi wa mafundi ngazi ya jamii na kuzidi kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wananchi na serikali,” lifafanua.
Kwa upande wake Hosiana Mawazo amesema umbali uliokuwepo kutoka Kijiji cha Iwihomelo kufuata huduma za afya umbali mrefu ulisababisha upatikanaji duni wa huduma za afya.
“Tunashukuru Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kutujengea kituo cha afya tunauhakika sisi wakinama tutapata huduma za afya karibu na maeneo tunayoishi na hivyo kutupunguzia gharama na adha ya kutembea umbali mrefu kupata huduma za afya ,” alieleza.
Hosiana ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kusogeza huduma za afya karibu haya ni maendeleo makubwa sana kwao.