Albano Midelo na Netho Sichali,Mbambabay
Wataalamu wa ujenzi kutoka Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma wameanza kikao kazi cha kuwajengea uwezo kuhusu usimamizi na ufuatiliaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi yote mwaka 2024/2025 inakamilika kabla ya Mei 30 mwaka huu.
Kikao kazi hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa St.Vinsenti mjini Mbambabay wilayani Nyasa ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma aliyewakilishwa na Mheshimiwa Peres Magiri ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa.
Akizungumza kabla ya kufungua kikao kazi hicho Mheshmiwa Magiri amewataka watalaamu hao wa ujenzi kuacha kukaa ofisini badala yake waende kusimamia miradi katika kila hatua ya utekelezaji ili iweze kukamilika kikamlifu na kwa wakati.
‘’Unakuta mradi unajengwa mtaalam wa ujenzi hajawahi Kwenda kukagua,wananchi wanaendelea na ujenzi ,hivyo mradi kupoteza ubora unaotakiwa,nawaomba baada ya kikao kazi hiki mbadilike’’,alisisitiza.
Amesema baada ya kukamilika kwa kikao kazi hicho anaamini kwamba miongoni mwa malengo yaliyokwekwa likiwemo la kumaliza ujenzi wa miradi ifikapo Mei 30 mwaka huu litafikiwa kwa kuhakikisha miradi yote wanayosimamia iwe imekamilika kulingana na maelekezo.
Awali akitoa taarifa kwenye kikao kazi hicho Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Girbert Simiya amekitaja kikao kazi hicho kinawahusisha watalaam wa ujenzi,wabunifu majengo na wakadiriaji majengo wa Mkoa wa Ruvuma waliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na katika Halmashauri zote nane.
Simiya amesema hadi sasa Mkoa wa Ruvuma una watalaamu 64 wa ujenzi kati yao wahandisi 20,wabunifu majengo watano,wakadiriaji majengo 11 na mafundi sanifu 28.
Ameitaja miradi inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Ruvuma kuwa ni Pamoja miradi ya barabara yenye tha
mani ya shilingi bilioni 70 na mradi wa ujenzi wa bandari ya Mbambabay wenye thamani ya shilingi bilioni 80.
Miradi mingine ameitaja kuwa ni miradi ya miundombinu ya elimu kupitia program ya BOOST yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 na program ya SEQUIP yenye thamani ya shilingi bilioni 14.6 na miradi ya program ya SWASH yenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni moja.
Katika kikao kazi hicho mada mbalimbali zitafundishwa zikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi.
Katibu Tawala Msaidizi Miundumbinu Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Girbert Simiya akizungumza kwenye kikao kazi cha wataalam wa ujenzi Mkoa wa Ruvuma katika ukumbi wa St.Vinsent mjini Mbambabay wilayani Nyasa
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kikao kazi cha wataalam wa ujenzi wa Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika mjini Mbambabay
Picha ya pamoja wataalam wa ujenzi wa Mkoa wa Ruvuma wakiwa katika kikao kazi na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri