NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Zaidi
ya washiriki 2000 wanatarajiwa kuchukua sehemu katika mbio za Kimataifa
za Utalii Kanda ya Ziwa (Lake Zone International Marathon 2025)
zitakazofanyika mkoani Mwanza.,kuhamasisha utalii na kuonesha fursa za
uwekezaji zilizopo mkoani humu.
Akizungumza na waandishi wa
habari, jijini Mwanza, leo Mkurugenzi wa Kilimanjaro One Sports
Promotion Ltd, Mohamed Hatibu, amesema kuwa mbio hizi zitafanyika
kuanzia Juni 27 hadi Juni 29, 2025, na zitakuwa na muktadha wa Tamasha
la Utamaduni linalotarajiwa kufanyika mkoani Simiyu.
Amesema kuwa
lengo la mbio hizo ni kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii
vilivyopo mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, ili kuchangia
katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa zima.
“Vivutio vya utalii
na fursa za uwekezaji katika Kanda ya Ziwa ni vingi, na ni muhimu kwa
Watanzania kuvitangaza ili kuvutia wageni na kuingiza fedha za kigeni
zinazosaidia maendeleo ya sekta mbalimbali,” amesema Hatibu.
Mkurugenzi
huyo ameongeza kusema kuwa utalii umeimarika kutokana na juhudi za
Serikali ya Awamju ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,
imefungua fursa na Diplomasia ya uchumi na kutangaza vivutio vya
Tanzania kwa dunia.
Hatibu ameipongeza serikali kwa kuhakikisha
kuwa nchi inakuwa sehemu salama kwa wawekezaji na kuimarisha amani, hali
inayochochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii na kueleza kuwa
mbio hizo zitahusisha makundi mbalimbali, wakiwemo wajawazito, watoto,
walemavu, wazee, na viongozi kutoka mikoa mbalimbali.
Pia,
kupitia mbio hizo, wananchi watahamasishwa kujitokeza kwa wingi na
kujiandikisha ili kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa
amani.
Rhoda Kabarua, Msimamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
Kanda ya Ziwa, amesema kwa kushirikiana na Kilimanjaro One Sports
Promotion, mbio hizo zitakuwa ni makakati wa kutangaza vivutio vya
utalii vya Mwanza ikiwemo Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na Makumbusho ya
Utamaduni wa Wasukuma Bujora.
Amesema michezo hutoa fursa ya
kukutanisha watu kutoka sehemu mbalimbali, hivyo mbio hizo zitakuwa na
manufaa kiuchumi na zitaongeza mapato ya mkoa kupitia utalii.
Kwa
upande wake, Bertha Nikundiwe, Mtaribu wa Huduma ya Afya ya Uzazi, Jiji
la Mwanza, amesema mbio hizo pia zitatoa nafasi ya kutoa elimu ya afya
ya wajawazito na umuhimu wa mazoezi katika kupunguza vifo vya watoto
wachanga na wajawazito.
Amesema wajawazito watashiriki kwa kutembea
kwa dakika 20 hadi 30 na kufanya mazoezi mepesi, ambayo yanafaida kwa
afya zao, ikiwemo kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza shinikizo la
damu, sukari na kupunguza uzito, huku akisisitiza licha ya faida hizo,
wanawake wenye matatizo ya kiafya yanayohusiana na mimba hawataruhusiwa
kushiriki.